TANZANIA ilikuwa na watu milioni 6.2, wasiojua kusoma na kuandika hadi mwaka 2002. Taarifa hiyo, ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Diana Chilolo (CCM). Katika swali lake, Chilolo alitaka kujua kama idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika imemalizika na mpango wa Serikali wa kuimarisha Elimu ya Watu Wazima.
Dk. Kawambwa alisema idadi hiyo ni kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ambayo ni sawa na asilimia 31.
Alisema watu wasiojua kusoma na kuandika, hawajamalizika na kwamba Sensa ya mwaka 2012 bado haijatoa mchanganuo wa watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu.
“Ili kuimarisha Elimu ya Watu Wazima, Serikali inatekeleza mambo mbalimbali, ikiwemo kuboresha mpango wa awali wa Elimu ya Watu Wazima kupitia programu ya ‘Ndiyo Naweza’ yenye lengo la kupunguza idadi ya wasiojua kusoma na kuandika nchini.
“Serikali inatumia uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa Mpango wa Uwiano Kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA), ambapo mpaka mwaka 2012 ulikuwa na jumla ya wanakisomo 907,771,” alisema Dk. Kawambwa.
Alisema juhudi za pamoja zinahitajika ili kuwaondolea wananchi kadhia ya kutojua kusoma na kuandika, huku akitoa wito kwa viongozi wa kada zote na wale wa taasisi zisizo za Serikali kujihusisha kikamilifu kuhamasisha jamii na kuleta msukumo mpya katika kutekeleza Mipango ya Elimu ya Watu Wazima nchini.
MTANZANIA
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment