![]() |
| Mwanamke wa Kiiran akitumbukiza kura yake katika mojawapo ya chaguzi za nchi hiyo |
Mamilioni ya wananchi wa Iran wanatarajiwa kuelekea kwenye vituo vya kupiga kura hapo kesho katika uchaguzi wa kumtafuta Rais wa nchi hiyo atakayetawala kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Raia wapatao milioni 51 wenye kustahiki kupiga kura nchini humo wanajiandaa kumchagua mmoja kati ya wagombea sita walio katika mchuano mkali wa kampeni uliokamilika hapo jana Jumatano.
Kabla ya kuelekea vituoni, utafiti wa maoni unaonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wanaostahiki kupiga kura watashiriki katika uchaguzi huo wa 11 kumchagua rais wao.
Maoni ya hivi karibuni yanaonesha kuwa uchaguzi huo wa urais unaweza kwenda mpaka raundi ya pili na kuwashindanisha wagombea wawili watakaokuwa na alama za juu.
Kwa sheria ya uchaguzi ya Iran, mgombea wa urais anatakiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote katika raundi ya awali ili aweze kushinda. Vinginevyo, wagombea wawili wa juu wakuchuana katika raundi ya pili inayotarajiwa kufanyika Juni 21.
Wagombea sita katika uchaguzi wa urais wa Iran ni mkuu wa Kituo cha Baraza la kulinda Maslahi ya Kitaifa kwa Utafiti wa Kistratejia Hassan Rohani, Katibu wa baraza kuu la Usalama wa Kitaifa Saeed Jalili, Katibu wa Baraza la kulinda maslahi ya Kitaifa Mohsen Rezaei, Meya wa mji wa Tehran Mohammad Baqer Qalibaf, waziri wa zamani wa mashauri ya kigeni Ali Akbar Velayati, na waziri wa zamani wa mawasiliano Mohammad Gharazi.
Kwa upande mwingine, Spika wa zamani wa bunge Gholam Ali Haddad-Adel na Mohammad Reza Aref, aliyewahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais, walijiondoa katika kinyang'anyiro hicho mapema wiki hii.

0 comments:
Post a Comment