RAIS WA UFARANSA APEWA TUZO NA UNESCO KWA KUINGILIA KIJESHI NCHINI MALI






Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na elimu, sayansi na Utamaduni, UNESCO, limempa Rais wa Ufaransa, Francois Hollande tuzo ya mwaka  ijulikanayo kama Tuzo ya Amani ya Felix Houphouet-Boigny kwa uamuzi wake wa kuingilia Mali kijeshi.

Hollande alipokea tuzo hiyo kubwa katika sherehe iliyofanyika katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris, jana Jumatano.


Hatua hiyo imeibua maswali mengi kuhusu jinsi uingiliaji wa kijeshi kutoka nje unavyoweza kustahili kupewa tuzo kama hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova alisema wakati wa sherehe hizo kuwa "sote tuna sababu ya kujivunia uamuzi wa Ufaransa kusimama upande wa Mali- kwa ombi la Rais Traore na kwa kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa – kuwalinda watu na utamaduni wa nchi ile.”


Naye Hollande akasema kuwa "Linaweza kuonekana kuwa jambo lenye kukanganya kupewa tuzo ya amani baada ya kuchukua jukumu la kuingia vitani.”

"Lakini uamuzi nilioufanya kwa niaba ya Ufaransa hakuwa na lengo lingine zaidi ya kukomesha hujuma," alisema.

Tuzo ya Amani ya Felix Houphouet-Boigny iliyoanzishwa mwaka 1989, ina lengo la kuwapa heshima watu na mashirika yaliyotoa “mchango mkubwa katika kuleta amani na uthabiti ulimwenguni.”


Wanajeshi wapatao 4,000 wa Ufaransa wamepelekwa nchini Mali tangu Januari 11 kwa hoja ya kwenda kukabiliana na wapiganaji waliokuwa wakilidhibiti eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.


Vita hiyo imesababisha mgogoro mkubwa wa kibinaadamu katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo na kuwahamisha maelfu ya watu ambao sasa wanaishi katika hali mbaya sana.

Mnamo Februari 1, Shirika la haki za binaadamu la Amnesty International lililaani “uvunjifu mkubwa wa haki za kibinaadamu” ikiwemo mauaji ya “watoto watatu” katika vita hiyo inayoongozwa na Ufaransa nchini Mali.


Shirika hilo la kutetea haki za binaadamu lilisema kuwa kulikuwa na “ushahidi kwamba kwa uchache raia watano, wakiwemo watoto watatu, waliuawa katika mashambulizi ya ndege” yaliyofanywa na vikosi vya Ufaransa dhidi ya wapiganaji wa eneo hilo.


Mwezi Aprili Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian alithibitisha kuwa nchi yake itawabakisha askari wake 1,000 nchini Mali hata baada ya kuwasili kwa askari 12,000 wa kulinda amani kutoka Umoja wa Mataifa.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa maliasili zilizojaa nchini Mali kama vile dhahabu na madini ya urani, zinaweza kuwa miongoni mwa sababu za uingiliaji kijeshi uliofanywa na Ufaransa.


Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment