MAOMBI YA VIONGOZI WA UAMSHO YATUPWA





MAHAKAMA ya Rufaa ya Tanzania, imetupilia mbali maombi ya viongozi wa dini wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya kutaka taarifa ya kukata rufaa iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), itupiliwe mbali. Maombi hayo yalitupwa mwishoni mwa wiki na jopo la majaji watatu, walioyasilikiza na kuahidi kutoa uamuzi baada ya kupitia hoja za pande zote mbili.


Jopo hilo ni Jaji Januari Msoffe (mwenyekiti), William Mandia na Salum Massati ambao katika uamuzi wao walisema walioleta maombi hawana hoja za msingi kisheria, hivyo waliamua kutupilia mbali maombi yao.


Awali Juni 10 mwaka huu mawakili wa viongozi wa dini, Salum Toufiq, Abdalla Juma, Suleiman Salum na Rajabu Abdalla waliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali taarifa ya kukata rufaa iliyowasilishwa na DPP kwa madai kwamba, haikuwa sahihi kwani itachelewesha kesi na kusababisha wateja wao waendelee kusota rumande kwa muda mrefu.


Akijibu hoja ya kutupa taarifa ya rufaa, Jaji Msoffe alisema katika kesi za madai kuna kanuni inayoruhusu kutupilia mbali taarifa hiyo, lakini katika jinai haipo.


“Kuna kesi gani ambayo ilishawahi kuamuliwa na taarifa ya kukata rufaa katika kesi ya jinai ikatupwa au mnataka kuanza na hii,” alihoji Jaji Msoffe.


Wakili Toufiq, alidai kwamba hana kumbukumbu ya kesi yoyote iliyowahi kuamuliwa, lakini kila jambo linakuwa na mwanzo hivyo kesi yao itakuwa ya kwanza.


Mawakili wa Serikali, waliomwakilisha DPP Rashid Abdallah, Ramadhan Nassib na Suleiman Haji walidai mahakamani kwamba, ili mtu afike mahakamani kuomba rufaa itupwe lazima awe na sababu nzito za msingi.


Katika hatua nyingine mawakili wa pande zote mbili walikubaliana kwa pamoja kwamba Msajili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, aliyesikiliza maombi ya kwanza ya dhamana ya Sheikh Farid na wenzake tisa, hakuwa na mamlaka kisheria ya kufanya hivyo.



Mbali ya Sheikh Farid, waleta maombi wengine ni Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Mussa, Azan Khalid, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman, Ghalib Ahmada Juma, Abdallah Said na Fikirini Fikirini.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment