KIKWETE AMSHIKA ‘PABAYA’ KAGAME


Rais wa Rwanda Paul Kagame


SHEREHE za miaka 50 ya Umoja wa Afrika (AU) zamani ukifahamika kama OAU hazikuwa njema sana kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambaye aliondoka Addis Ababa, Ethiopia akiwa amenuna.

Kagame, mpiganaji wa zamani wa msituni aliyeshirikiana bega kwa bega na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kuung’oa utawala wa Milton Obote na baadaye Jenerali Tito Okello mwaka 1985, anadaiwa kukwazwa na ushauri ‘wa wazi’ aliopewa na Rais Jakaya Kikwete kuhusu njia ya uhakika ya kuleta amani ukanda wa Maziwa Makuu.

Wakiwa kwenye sherehe hizo, Kikwete aliwaambia waziwazi Kagame, Museveni na Rais wa Kongo, Joseph Kabila kuwa wanapaswa kufanya mazungumzo na ‘waasi’ wenye silaha wanaopingana nao kutafuta njia ya kupata utatuzi wa kudumu wa migogoro na umwagaji damu katika eneo la Afrika.

Mbele ya marais wengine 11 na wawakilishi wa nchi kadhaa za Afrika, Luteni Kanali (mstaafu) Kikwete alimtaka Jenerali (mstaafu) Kagame kuzungumza na waasi wa Kinyarwanda waliojificha kwenye jimbo la Kivu, waitwao Democratic Liberation Forces of Rwanda (FDLR).

Kanali Kikwete akamwomba Jenerali Museveni azungumze na Allied Democratic Forces/National Army for Liberation of Uganda (ADF/NALU) wanaoipinga serikali yake huku akimtaka Jenerali Joseph Kabila kuzungumza na waasi wa M23.

Naam, ni maelekezo hayo halali kabisa kutoka kwa ‘Kanali’ kwenda kwa ‘Majenerali’ ndiyo yaliyomkasirisha Jenerali Kagame ambaye hakuzungumza lolote mbele ya marais wengne pale Addis Ababa, akabaki nalo moyoni hadi Kigali!

Kikwete anaamini kuwa hata askari aliowapeleka DRC kulinda amani hawataleta amatunda ya maana iwapo marais hawa hawatakaa mezani na waasi wao kutafuta njia ya kumaliza migogoro inayoonekana kuwa ya kudumu kwa sasa.

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa AfroAmerica, kauli ya Kikwete si mpya kama inavyodhaniwa na wengi, kwani mtandao huo umewahi kuitoa katika machapisho yake kadhaa hasa lile la Machi 7, mwaka huu lililouliza iwapo Rais Kagame wa Rwanda atatumia fursa ya uwapo wa Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa mtaifa ukanda wa Maziwa Makuu kumaliza vita kwenye ukanda huo.

“Cha kushangaza ni kwamba safari hii maneno hayo yametoka mdomoni mwa mmoja kati ya marais wenye ushawishi mkubwa barani Afrika. Ukweli ni kwamba, pamoja na Rais wa Angola, Jose Eduardo Dos Santos na wa Afrika Kusini Jacob Zuma, huenda Kikwete kwa sasa ndiye Rais muhimu zaidi katika kizazi hiki cha Afrika.

“Marais hawa watatu ndio watu wenye busara ambao jumuiya ya kimataifa huwasiliana nao kabla ya kufanya jambi lolote kubwa linalohusu nchi za maeneo ya Kati, Mashariki na Kusini mwa Afrika. Na wala si ajabu kuwa Obama atazitembelea Tanzania na Afrika Kusini (na kusimama kwa muda Senegal) baadaye mwezi huu,” inasomeka sehemu ya mtandao huo wa AfroAmerica.

Jijini Addis, Jenerali Museveni alijibu kuwa atafanya mazungumzo na wale walio tayari na kuachana na wengine huku Jenerali Kagame akinyamaza kimya; lakini kwa vyovyote iwavyo, ujumbe kwa marais hawa wapiganaji wa msituni umewafikia, uamuzi wa kufanya au kutofanya mazungumzo na wapinzani wao uko mikononi mwao.

Kauli ya Kikwete imezua mijadala mikubwa ndani na nje ya Tanzania, wengine wakiiunga mkono huku wengine wakiilani na kutaka amwombe radhi Jenerali Kagame, waathirika wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 na Wanyarwanda wote kwa ujumla.

Mijadala hiyo inaonesha maana moja tu; kwamba Kikwete ‘amemshika pabaya’ Kagame na wale wanaomuunga mkono. Hii ni kwa kuwa hakuna kinachozungumzwa kuhusu Uganda na DRC zaidi ya Rwanda kana kwamba ni Kagame pekee aliyeshauriwa kufanya mazungumzo na waasi.

Katika kuonesha jinsi Jenerali Kagame, aliyezaliwa Oktoba 27, 1957 Kusini mwa Rwanda, alivyokasirishwa na kauli ya JK, mtandao wa AfroAmerica unaandika:

“Msimamo wa Kikwete umewakera sana viongozi wa Rwanda kiasi kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo na Waziri wa ulinzi, James Kabarebe, waliilani hadharani na kumwita Kikwete ‘mtu anayewahurumia wahusika wa mauaji ya kimbari’, ‘aliyeyakana mauaji hayo’ na majina mengine mabaya.

“Bado haijafahamika kama katika siku za karibuni Kikwete na Kagame watakaa na kulijadili suala hilo. Kwa mujibu wa vyanzo kutoka Rwanda, Jenerali Kagame aliporejea kutoka Addis, alionekana wazi kujawa na hasira.

“Akaamuru kufanyika kikao cha dharura cha idara ya Usalama wa Taifa na kuwaambia washiriki kwa Kinyarwanda kuwa Kikwete ni ‘Four Bs’, akimaanisha kuwa ni ‘mbabaishaji’ (opportunist), ‘mpenda sifa’, ‘mjivuni’ na ‘mtu asiyefaa’.

“Lakini kinyume na tabia yake, Kagame alivunja mkutano huo baada ya dakika 15 na moja kwa moja akaenda kulala.

“Kabla hajaondoka kuelekea Japan (kwenye mkutano na waziri mkuu wa huko ambaye pia alimwalika Kikwete), Kagame aliitisha tena mkutano wa idara ya usalama wa Taifa na maofisa wa juu wa jeshi akawaambia …’Sasa, baada ya usaliti wa huyo jamaa wa Tanzania, ni wazi kwamba, kama watoto yatima, tupo peke yetu. Ninaondoka, nitakaporudi ninataka mnipe mpango jinsi gani tutaondokana na hali hii mbaya.’

“Alipouliza kama kuna mwenye nyongeza, wote walitazama chini. Akavunja mkutano na kukwea ndege binafsi aliyoikodi serikalini.”

Kagame aliyekwea ngazi za kijeshi hadi ujenerali, alijifunza masuala ya ujasusi (espionage) nchini Tanzania wakati huo yeye na rafikiye Fred Rwigyema wakiwa askari wa serikali mpya ya Uganda chini ya Museveni.

Meja Rwigyema, rafiki wa utotoni wa Kagame, alipigana vita ya Kagera akiwa na Museveni mwaka 1979.

Paul ni mtoto wa mwisho kati ya watoto sita wa familia ya Deogratias Kagame, Mtutsi aliyekuwa na undugu na Mfalme Mutara III, lakini akaamua kuwa mfanyabiashara.

Mama yake Jenerali Kagame, Asteria Rutagambwa, anatoka kwenye familia ya malkia wa mwisho wa Rwanda, Rosalie Gicanda.

Mauaji yaliyotokana na Mapinduzi ya Rwanda mwaka 1959 dhidi ya Watutsi yaliilazimisha familia ya Kagame kukimbilia Kaskazini mwa Rwanda, wakavuka mpaka na kwenda kuishi kwenye kambi ya wakimbizi ya Nshungerezi, Uganda, mwaka 1962, na ni kipindi hicho walipokutana na Rwigyema.

Kagame alisoma shule ya msingi karibu na kambi hiyo na yeye pamoja na Wanyarwanda wengine walipoanza kujifunza Kiingereza na kujichanganya na tamaduni za Uganda.

Akiwa na miaka tisa, alijiunga katika shule ya msingi iliyokuwa ikiheshimika sana wakati huo, Rwengoro, kilomita 16 kutoka kambini na kufaulu kwa alama bora zaidi wilayani humo, kisha akajiunga katika shule bora ya sekondari Ntare, nchini Uganda, ambayo alisoma Museveni pia.

Kifo cha ba yake, mwanzoni mwa miaka ya 1970 na kuondoka kwenda kusikojulikana rafiki yake Rwigyema kulishusha kiwango chake cha elimu na kuzidisha tabia ya kupambana na waliokuwa wakiwadharau Wanyarwanda, baadaye akafukuzwa Ntare na kumalizia katika shule ya sekondari Old Kampala kwa kiwango cha kawaida.

CHANZO: RAI

Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

1 comments:

  1. Hawa watu Watutsi wana agenda yao, agenda hiyo JK wa zamani alikuwa ndiye mlezi wa mtandao huo, JK wa sasa anaujua na ni mmoja wapo wa watakaoathirika yeye na kizazi chake, kama itakavyokuwa kwa kila asiye na asili ya kitutsi anayeishi ktk eneo la maziwa makuu....So nina uhakika kuna zaidi ya kauli hiyo, kwani kwa kauli hiyo tu aitoshi kumtia hasira na jazba Rais Kagame kiasi hicho...nina uhakika anajua kuwa JK huyu wa sasa ni mtu wa namna gani, anajua upeo wake na tayari kuna hali ambazo zinajionesha wazi kuwa JK anataka amani ya kweli kwenye eneo hili la maziwa makuu, kitu ambacho watutsi hawakitaki, wanataka pasitulie huku wao wanatengeneza hujuma za kulikamata eneo hili..DRC inatakiwa kuwa ndiyo sehemu itakayotayarishiwa jeshi kubwa litakaloweza kupambana na Tanzania, kwa sasa jeshi hilo eti ndiyo hayo makundi ya waasi, kwa mazoezi wanayoyafanya, kuyapambanisha na ya serikali si muda mrefu ujao watakuwa na uwezo wa kupambana na Tanzania, nchi ambayo ndiyo iliyobaki kuwa kikwazo ktk kutimiza lengo lao ingawa huko nyuma ndiyo ilikuwa mhimili wa mtandao huo bila waTanzania wa kawaida kujua kinachoendeleo...tumesoma nao, tumefanya nao kazi tena ktk taaluma na nyadhifa adhimu hapa kwetu Tanzania...Nampongeza Rais JK na namuomba akaze buti kwani tulipofikia panatisha. Hata jumuiya ya Afrika mashariki ni mtego ktk hili, Kenya analiangalia kiuchumi zaidi huku akijipanga kuitumia Tanzania kama kiwanda chake na shamba la kukuzia uchumi wa Kenya, NA kwa kuwa yeye Kenya hahusiki na mpango wa Watutsi, kwani yeye hayumo ktk eneo la maziwa makuu, hajali hilo......Uganda imeshashikwa kiuno, haikukuruki utiifu wake kwa waTutsi uko wazi kuanzia jeshini mpaka kwenye taasisi za fedha za Uganda...Baada ya yote hayo, watutsi lengo lao kwenye jumuiya ni kuiingia vyema Tanzania ili wapate fursa ya kutekeleza agenda yao. JK ANAJUA AND HE IS ACTING AGAINST THEIR PLAN....

    ReplyDelete