Marekani imezidi kuibana Iran kuwa kupanua vikwazo dhidi ya sarafu ya nchi hiyo na sekta ya viwanda vya magari kutokana na programu yake ya nishati ya nyuklia.
Juzi Jumatatu, Rais wa Marekani, Barack Obama alisaini waraka maalumu wa kupanua vikwazo vya sasa vilivyowekwa dhidi ya Iran.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jay Carney alisema, “Hatua hii mpya inailenga sarafu ya Iran, yaani RIAL, kwa kuidhinisha vikwazo dhidi ya taasisi za fedha za kigeni ambazo kwa makusudi zitafanya au kuwezesha miamala kwa mauzo au manunuzi ya sarafu ya Iran, au zile zitakazoendelea kuwa na akaunti muhimu nje ya Iran na kuwa na pesa nyingi za sarafu ya Iran.”
Vilevile, ongezeko hilo la vikwazo linahusu manunuzi au usafirishaji wa bidhaa au huduma zinazopelekwa kwenye sekta ya magari ya Iran.
Hatua hizo zimepitishwa na Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Marekani tarehe 22 Mei.
Mnamo Mei 31, Hazina ya Marekani ilitoa taarifa, ikitangaza vikwazo dhidi ya makampuni 8 ya mafuta na kemikali ya Iran kama vile Bou Ali Sina, Mobin, Nouri, Pars, Shahid Tondgouyan, Shazand, Tabriz na Imam.
Mwanzoni mwa mwaka 2012, Marekani na Jumuiya ya Umoja ya Ulaya ziliweka vikwazo vipya dhidi ya ya sekta za Iran za mafuta na fedha kwa lengo la kuzizuia nchi nyingine kununua mafuta ya Iran na kufanya miamala na Benki Kuu ya Iran.
Marekani na Ulaya zinaituhumu Iran kwamba programu yake ya nishati ya nyuklia inalenga kuzalisha kuzalisha silaha za nyuklia.
Iran imekuwa ikikanusha madai na tuhuma hizo na kushikilia msimamo wake kuwa ina haki ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani na miradi ya kiraia kwa kuwa nchi hiyo ni mwanachama aliyeweka saini kwenye Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia ueneaji wa silaha za Nyuklia (NPT) na ni mwanachama wa Wakala wa KImataifa wa Nishati ya Atomi (IAEA).
0 comments:
Post a Comment