*WAPIGA KURA 25 WATEKWA, MAPANGA, MARUNGU YARINDIMA
*KIGOGO UVCCM AKAMAWATWA NA BASTOLA, DC AZUA JAMBO
*KIGOGO UVCCM AKAMAWATWA NA BASTOLA, DC AZUA JAMBO
UCHAGUZI mdogo wa madiwani katika kata 22, uliofanyika jana nchini ulitawala na vurugu, vipigo, kutekwa, huku baadhi ya viongozi wa kisiasa wakikamatwa. Uchaguzi huo mdogo umeonekana kutawaliwa na matukio mabaya, jambo ambalo limewafanya wananchi wengi katika maeneo hayo kuwa na wasi wasi.
Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na kupigwa, kujeruhiwa na kuumizwa kwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA), aliyelazwa katika Hospitali ya Selian, jijini Arusha.
Taarifa kutoka Arusha zinasema kuwa, Nassari alipatwa na mkasa huo baada ya kudaiwa kumpiga kofi na kumtishia kwa bastola wakala wa CCM katika Kijiji cha Saburi Kata ya Makuyuni.
Tukio hilo, lilitokea jana saa 4 asubuhi, wakati kazi ya upigaji kura ikiendelea, ambapo Nassari alikwenda moja kwa moja hadi ndani ya kituo cha kupigia kura.
Chanzo hicho kilisema, akiwa ndani ndipo mabishano yalipozuka kutoka kwa wafuasi wa vyama vya CCM na CHADEMA. Hata hivyo haikuweza kufahamika mara moja chanzo cha mabishano hayo.
SERENGETI
Habari kutoka wilayani Serengeti mkoani Mara, zinasema Jeshi la Polisi linamshikilia Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Tarime, Boniface Mhele kwa kosa la kukutwa na bastola.
Mhele alikutwa na silaha hiyo katika kituo cha kupigia kura cha Butengi kinyume cha sheria.
Mbali ya kukamatwa kiongozi huyo, vijana 25 wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilayani humo wametekwa na haijulikani walipo hadi sasa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Serengeti, OCD Pius Ngoko alisema hadi jana jioni Mhele alikuwa akishikiliwa na Polisi.
“Tunamshikilia Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Tarime kwa mahojiano zaidi, kwa sababu amekutwa na bastola kwenye kituo cha kupigia kura jambo ambalo ni hatari.
“Alifikishwa kituoni hapa na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambao walimkamata baada ya kumshtukia,” alisema OCD Ngoko.
Kuhusu malalamiko ya CHADEMA, kuwa kuna vijana zaidi ya 25 waliotekwa na kikosi cha watu wasiojulikana.
Kamanda huyo alithibitisha tukio hilo linalomhusisha Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo, Joshua Mirumbe, kama kiongozi wa genge la watekaji.
“Nimesikia kuna vijana wametekwa, siwezi kuliongelea kiundani zaidi, nimewaomba wale wote wanaolalamika waende kituoni watasikilizwa, sijui kama ni DC huyo ngoja tuendelee kufuatilia,” alisema.
Alipoulizwa kuhusiana na kitendo cha DC Mirumbe kutumia askari magereza kukamata vijana wanaoonekana kuunga mkono upinzani, kamanda huyo hakukataa wala kukubali.
“Ni kweli nimepewa oda ya kukamata watu, lakini sioni kama kuna sababu hiyo, hali ni tulivu, inawezekana DC mwenyewe ndiye anajua mambo mengine,” alisema OCD.
Kuhusu kilio cha wafuasi wa CHADEMA, kuwa kuna vijana wanaotumiwa na CCM chini ya Mirumbe, OCD Ngoko alisema muda wote wamejipanga kudhibiti wavunja amani.
HECHE ALONGA
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA), John Heche ambaye anasimamia uchaguzi huo, alisema mpaka jana mchana hali ilikuwa mbaya.
“Pamoja na kufanikiwa kukamata viongozi wa CCM, vijana wetu wengi wamekamatwa na DC Mirumbe, anatumia askari magereza sijui ametoa wapi jeuri hii,” alisema Heche.
Alisema muda wote DC Mirumbe, alikuwa anatumia gari lenye namba za usajili STK 8430 na jingine ni aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba T622BFJ.
Alitaja magari mengine ambayo yalikuwa yakiendesha operesheni hiyo kuwa ni aina ya Toyota Land Cruiser zenye namba za usajili T286, T545, T573 na T352.
“Kijana wetu, Amos Manginare tumemuokota porini katika Kijiji cha Miseke saa 7 mchana, hali ni mbaya.
Aliwataja vijana waliotekwa na vijiji vyao kwenye mabano kuwa ni Berena Maro (Bwitengi), Samson ogao (Rwamchanga), Adam Samson (Bwitengi), Emannuel Eliya (Bwitengi), Onyango Otaro (Miseke), Manginare Samsoni (Miseke), Elija Wilson (Miseke) na Banage Nanai (Rwamchanga).
Wengine ni Matororo Saina (Rwamchanga), Pikipiki Simba (Rwamchanga), John Oninga (Rwamchanga), Richard Christopher, Baraka Nestory, Mwalimu Makima na Peter Odoa.
SENGEREMA
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mji wa Sengerema jana ulionekana kuwa uwanja wa vita, baada ya watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa CCM, kuwafyatulia risasi za moto viongozi na makada wa Chadema.
Tukio hilo lilitokea jana saa 4 asubuhi, katika uwanja wa mpira wa Shule ya Msingi, Sengerema mjini hapa, wakati wafuasi wa CCM na Chadema walipokutana.
Walikutana wakiwa wanafuatilia hali ya mambo katika vituo vya kupigia kura katika uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Nyampulukano.
Katika tukio hilo, milio ya risasi zaidi ya mine ilisikika kutokea upande wa pili wa CCM, ambapo magari matatu yalilizunguka gari moja lililokuwa likitumiwa na baadhi ya viongozi wa Chadema.
Ndani ya gari hilo alikuwemo kiongozi wa Chadema Kikosi cha Movement for Change (M4C), Kanda ya Ziwa Magharibi, Alfonce Mawazo, Hussina Amri na makada kadhaa.
Baada ya gari la Chadema kuzingirwa na magari matatu ya CCM na baadaye risasi za moto kufyatuliwa hewani, wananchi waliokuwa maeneo hayo walilazimika kuingilia kati kwa kupambana na wafuasi hao wa CCM.
Vurugu hizo za uchaguzi zilianza kutokea usiku wa kuamkia jana, ambapo inadaiwa wafuasi wa Chadema walitekwa na magari mawili yaliyokuwa na watu wanaodhaniwa kuwa na wafuasi wa CCM.
Wakizungumzia matukio hayo Mawazo na Mbunge wa Nyamagana Ezekiel Wenje walilaani kitendo cha CCM kutumia nguvu kwa lengo la kutaka ushindi.
“Wakati tulipofika uwanja wa shule ya msingi Sengerema, ghafla yalikuja magari matatu ya wafuasi wa CCM kisha yakatuzunguka nyuma, mbele na ubavuni.
“Katika prukushani hizo wafuasi wa CCM walifyatua risasi zaidi ya nne hewani, na baada ya kuona hivyo wananchi waliokuwa maeneo hayo wakaanza kuwapiga mawe ndipo walipotimua mbio,” alisema Mawazo.
Naye Wenje alisema: "CCM wanafanya hivyo kwa kuelewa kabisa kwamba hawatashinda. Kwa hiyo wanalazimika kutumia nguvu kubwa kutafuta ushindi wa nguvu...wananchi walishawakataa hata wafanyeje hawatoki,” alisema.
Maofisa wa polisi wilayani hapa wamethibitisha kutokea kwa matukio hayo, ambapo walisema kuna baadhi ya wafuasi wa CCM wamekamatwa wakiwa na mapanga.
Taarifa za awali zilidai kwamba, kati ya vituo 12 vya kupigia kura kata hiyo ya Nyampulukano, karibu zaidi ya nusu yake Chadema walikuwa wakiongoza, huku wakifuatiwa kwa karibu na CCM.
MATUKIO
Taarifa kutoka katika maeneo mbalimbali nchini ambapo uchaguzi huo ulifanyika jana, zilieleza kuhusu kukithiri kwa vitendo vya shari na hujuma.
Matukio hayo yamelaaniwa na baadhi ya vyama vya siasa, kwa maelezo kuwa havina tija wala afya kwa mustakabali wa taifa.
KATA YA IYELA
Katika kata hiyo gari la CCM lenye Usajili namba T 704 BEU, likiwa na watu wawili wanaotambulika kwa majina ya Moris na Nosy, wanadaiwa kuwateka vijana wa CHADEMA.
Kijana mmoja kati ya hao anadaiwa kuumizwa vibaya kwa kuchomwa kisu.
Ofisa Mwandamizi wa Chadema, Erasto Tumbo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, huku akimtaja kijana aliyechomwa kisu kwa jina la Meshack Bernard.
“Vijana wa CCM waliokamatwa wameachiwa huru na jeshi la polisi na sasa wanatumia gari nyingine yenye rangi nyekundu Toyata Surf namba T-173 ANE, wakiendelea kufanya vitendo viovu.
“Katika kituo cha kupigia kura cha SIDO ,vituo 3 vimelundikwa sehemu moja na eneo hilo kuna Karakana ambayo inawafanya watu kuingia na kutoka kinyume na sheria za uchaguzi,” alisema.
KATA YA MABALAMAZIWA
Katika kaya hiyo watu sita wanadaiwa kupigwa kwa marungu na visu na kuumizwa vibaya wakati zoezi la upigaji wa kura likiendelea.
KATA YA MINEPA, MOROGORO
Tukio lililotokea huko ni kuchomwa moto PIKIPIKI mali ya Chadema na vijana wa CCM (greenguard).
Taarifa zinaeleza kuwa katibu wa chama hicho wilaya ndugu Lucas Daniel amepigwa na kuumizwa na mwenzake amekatwa vidole.
KATA YA MIANZINI, DAR
Tukio lililotokea mjini humo ni kutekwa kwa wanachama na kiongozi wa Chadema, ambapo watu hao walitekwa na kufungwa vitambaa vyeusi machoni.
Mmoja kati ya vijana hao ni Katibu wa Vijana CHADEMA Tawi la Machinjioni anayeitwa Julius Vedastua na mpaka sasa amelazwa hospitalini.
Hali kadhalika kwa baadhi ya maeneo katika kata hii ni kuwa na wasimamizi wengi katika kituo kimoja na wasimamizi hao wamekuwa wakiwaongoza watu kupiga kura mpaka kwenye ile sehemu ya kupigia kura na kuwapa maelezo juu ya nani wa kumchagua, kitendo ambacho ni kinyume na Sheria.
KATA YA STESHENI, LINDI
Taarifa zilizolifikia gazeti hili ni kwamba magari ya CCM yanadaiwa kusomba wapiga kura na kati ya magari yanayotumika ni gari lenye za usajili T670 DEU.
KATA YA DONGOBESH, MANYARA
KATA YA DONGOBESH, MANYARA
Katika kata hiyo, makada wa CCM wanadaiwa kuvamia katika vilabu vya pombe na kuwanunulia wananchi pombe kama hongo ya kutaka chama chao kupigiwa kura.
Msemaji wa Chadema, amesema baada ya kuwanunulia pombe makada hao wamekuwa wakiwasomba kwa magari na kuwapeleka katika vituo vyao vya kupigia kura.
CHANZO: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment