Watumishi wa Serikali kupata mikopo ya nyumba kuanzia September, 2013.


THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Watumishi wa Serikali kupata mikopo ya nyumba
kuanzia Septemba, 2013.
Watumishi wa Serikali, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, kuanzia Septemba mwaka huu wataanza kunufaika na mikopo nafuu ya ujenzi wa nyumba za kuishi chini ya utaratibu mpya ulioandaliwa na Serikali na unaojulikana kama Mpango Maalum wa Nyumba za Kuishi za Watumishi wa Umma – Public Servant Housing Scheme.
Mpango huo ulitangazwa , Ijumaa, Mei 17, 2013 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa hotuba yake ya kufunga Wiki ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwenye bustani ya Nyerere Square mjini Dodoma.
Hata kabla ya kuutangaza Mradi huo hadharani mjini Dodoma, Rais Kikwete alikwishakuambiwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Beno Ndullu kuwa chini ya Mpango huo, watumishi wa Serikali kuanzia Septemba mwaka huu wataweza ama  kukopa nyumba za gharama nafuu ama kukopa mikopo ya gharama nafuu ambayo italipwa katika kipindi cha miaka 25.
Gavana Ndullu alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum iliyoteuliwa na Rais Kikwete kuangalia jinsi gani ya kuwasaidia watumishi wa Serikali katika Tanzania kuweza kupata mikopo nafuu ama kukopa nyumba za bei nafuu ambayo iliwasilisha ripoti yake kwake katika mkutano uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam katikati ya wiki iliyopita.
Chini ya mpango huo, ambao utaendeshwa na kampuni iitwayo Watumishi Housing Company Limited iliyoandikishwa na kupewa usajili Februari mwaka huu, 2013, kiasi cha nyumba 5,000 zitajengwa katika miaka ya kwanza mitano, mwaka wa kwanza zikiwa zimejengwa nyumba 2,500.
Mpaka sasa kiasi cha Sh. bilioni 68 zimekwishapatikana kati ya kiasi cha Sh.bilioni 358 zinazotarajiwa kuwekezwa katika Mradi huo katika miaka hiyo mitano ya mwanzo na itakuwa ni kampuni hiyo ambayo itajenga nyumba za gharama nafuu na kuwezesha kupatikana kwa mikopo nafuu kwa watumishi ambao watapendelea kukopa fedha ili kujenga wenyewe nyumba za kuishi.
Taasisi zitakazoshiriki katika kampuni hiyo ni pamoja na mifuko ya Hifadhi ya jamii ya NSSF, PPF, PSPF, LAPF, GEPF, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Mbali na taasisi hizo, pia benki 10 zimekubali kushiriki katika Mradi huo. Mabenki hayo ambayo yatakuwa yanatoza riba ya kati ya asilimia 10 na 13 kwa miaka yote 25 ya mkopo ni NMB, CRDB, NBC, Bank of Africa, Azania Bank, EXIM Bank, Banc ABC, NIC Bank, DCB Bank na KCB.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
20 Mei, 2013
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment