JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha,linaendelea kuwafanyia uchunguzi watuhumiwa wa mlipuko wa bomu katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti Arusha. Akizungumza ofisini kwake juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,Liberatus Sabas alisema watuhumiwa ambao bado hawajafikishwa mahakamani wanaendelea kufanyiwa uchunguzi.
“Hatutaki kumuonea hata mtu mmoja, tunahitaji kufanya uchunguzi wa kina ili tutende haki,” alisema ACP Sabas.
Hata hivyo, alipoulizwa endapo watuhumiwa kama bado wapo rumande kwa mahojiano, alisema sheria haziruhusu watuhumiwa hao kuendelea kukaa rumande.
“Tumewapa dhamana kwa masharti ya kuripoti polisi tunapowahitaji kwa mahojiano na uchunguzi zaidi,” alisema ACP Sabas.
Wakati watuhumiwa hao, wakiendelea kufanyiwa uchunguzi wa kuhusika na tuhuma hizo tayari mtuhumiwa mmoja Victor Ambrose amefikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya kuua na kukusudia kuua.
Watuhumiwa waliokuwa wakiendelea kushikiliwa kwa uchunguzi zaidi, ni Jassini Mbarak (29) mkazi wa Bondeni Arusha, Joseph Lomayani (18) dereva wa pikipiki mkazi wa Kwa Mrombo Arusha, Bathoromeo Silayo (23) mfanyabishara mkazi wa Olasiti, na Mohamed Suleiman Said (38) Mkazi wa Ilala Dar es Salaam.
Hata hivyo, watuhumiwa wengine katika sakata hilo ambao ni raia wa Nchi za Falme za Kiarabu waliachiwa huru, watu hao ni Abdulaziz Mubarak (30) Mkazi wa Falmae za Kiarabu, (Saudi Arabia).
Wengine ni Foud Saleem Ahmed (28) Raia wa Falme za Kiarabu, Said Mohsen mkazi wa Falme za Kiarabu (Najran) na Said Abdallah Said (28) Raia wa Falme za Kiarabu (Abudhabi).
Tukio la kurushwa kwa bomu hilo lilitokea Mei 5, Mwaka huu, Saa 4.30, na kusababisha vifo vya watu na kujeruhi wengine 66 waliopatiwa matibabu hospitali za Jiji la Arusha na Muhimbili Dar es Salaam.
Katika ibada hiyo ya uzinduzi wa Parokia mpya ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi iliyokuwa inazinduliwa na mgeni rasmi Balozi wa Vatcan nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Padilla akisaidiana na Askofu wa Jimbo Kuu la Arusha Joseph Lebulu.
CHANZO:MTANZANIA
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment