Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa kimegundua mipango iliyodai imeratibiwa na Serikali ya CCM ya kutaka kuwakamata na kuwatesa viongozi wa juu wa chama hicho, kwa madai ya kuhusika kuchochea vurugu za Mtwara.
CUF pia wamesema hatua hiyo haitasaidia kupunguza joto la wananchi hao, kwa kuwa chimbuko la mgogoro wa gesi katika mikoa ya Lindi na Mtwara ni kushindwa kwa Serikali ya CCM kutekeleza ahadi za miradi ya kutumia gesi ya Msimbati, Mnazi Bay na ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa megawati 300.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, aliwaambia wanahabari jana jijini Dar es Salaam kuwa chama chake kinafahamu kwamba Serikali ya CCM imezoea kubambikia watu kesi nzito wasizokuwa na hatia nazo.
“Kutukamata sisi siyo tatizo kwani haitasaidia kupunguza joto na hasira za wana-Mtwara, kinachotakiwa kufanywa na Serikali ni kutafuta chimbuko la mgogoro huo. Serikali ya CCM ndiyo imeutaka kwa kutoa ahadi hewa na za kisiasa bila kuzitekeleza,”alisema Lipumba na kuongeza: “Bunge limeshindwa kusimamia Serikali na kuhoji nini mradi wa kufua umeme wa MW300, ambao katika mwaka 2011/12 ulitengewa kutumia Sh540 milioni umesitishwa.”
Lipumba alisema kwamba CUF inafanya siasa kwa kujenga hoja na siyo kutafuta malumbano yasiyo na tija, hivyo hawahofii vitisho vya kukamtwa.
Alibainisha kuwa wamegundua mpango huo wa kuwakamata na kuwatesa kwa kuwahusisha na uchochezi wa vurugu hizo, akisisitiza kuwa msimamo wa chama chake upo palepale na kwamba Serikali inapaswa kutafuta chimbuko la mgogoro huo na siyo kutumia siasa.
Profesa Lipumba alisema kuwa Serikali inapaswa kuweka wazi mikataba yote inayohusiana na gesi ya mikoa ya Mtwara na Lindi haraka ili kila Mtanzania afahamu kilichokubaliwa kati yake na wawekezaji hao wa gesi.
“Sisi tunaitaka Serikali iweke wazi mikataba yote ya gesi ya Mtwara ili kila Mtanzania afahamu kitu gani kilikubaliwa kwenye mikataba hiyo na kwamba inapaswa iainishe wazi upembuzi yakinifu uliofanywa na mambo gani yalifikiwa katika upembuzi huo.”
Alisema kuwa ni vyema ikafahamika wazi kwamba madai makubwa ya wananchi wa Mtwara ni kutaka Serikali itekeleze miradi ya gesi waliyoahidiwa na siyo kuwalisha ‘sumu’ wananchi wa mikoa mingine kwamba wana-Mtwara hawataki rasilimali ya gesi iwafikie.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba amewataka polisi kuacha kutumia nguvu katika kurejesha amani ya Mtwara, akisema vitendo hivyo vinakiuka misingi ya haki za binadamu.
“Wananchi wanapigwa na kufanyiwa vitendo vya kinyama na Polisi sasa tunawataka waache kutumia nguvu zisizo hitajika kwani kuwapiga wananchi ni kukiuka misingi ya haki za dinadamu,”alisema.
Aidha, Lipumba alitoa pole kwa familia za watu waliopoteza ndugu zao katika vurugu hizo na kuwataka kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu.
chanzo:gazeti la mwananchi
chanzo:gazeti la mwananchi
0 comments:
Post a Comment