'Mawaziri wanauza dawa za kulevya'

Tuhuma mawaziri kuuza dawa za kulevya balaa


  Mbunge sasa 'asakwa' kiaina
  Pinda akwepa, awasafisha
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola
Serikali imembana Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, kwa kumtaka awasilishe ushahidi kuthibitisha kuwa baadhi ya mawaziri wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya mbunge mmoja kuitaka serikali itoe kauli kutokana na madai kwamba mawaziri wake wanajihusisha na biashara hiyo haramu.

Mbunge wa Tumbe (CUF), Rashid Ally Abdallah, alitaka kauli ya serikali jana alipouliza swali la papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema kuwa mbunge aliyetoa tuhuma hizo apeleke ushahidi, ili upelekwe kwa Rais.

Katika swali lake Abdallah, alisema kuwa Lugola alitoa kauli akisema wapo baadhi ya mawaziri wanaojishughulisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, licha ya wabunge hao kulindwa na ibara ya 100 ya katiba.

Abdallah alisema kauli hiyo ni nzito na inapaka matope serikali. “Waziri Mkuu anawaambia nini wabunge na wananchi kwa ujumla?” alihoji.

Akijibu swali hilo, Pinda alisema: “Mimi ni mmoja wa watu wazima, tunajua kauli anazozitoa mbunge zimepimwa vizuri kabla hajasema jambo lolote. Ninachoweza kusema ni kwamba mawaziri hawa kabla hawajateuliwa mchakato wake ni mgumu kidogo, Rais lazima ajiridhishe kwa mambo mengi, sasa kama mwenzetu aliyasema hayo kazi yangu mimi ni kusema si kweli.”

“Kwa sababu umeliuliza nataka nikubaliane na wewe kabisa, tumuombe tu Lugola sasa atuletee tu maelezo, ushahidi wowote wa waziri anayejishughulisha na madawa ya kulevya, sisi tutapeleka maelezo hayo kwa Rais, hatua stahiki zitachukuliwa,” aliongeza Waziri Mkuu.

Mbunge huyo alimtaka Waziri Mkuu amwombe Naibu Spika, Job Ndugai, amtake Lugora athibitishe kwa kutoa ushahidi bungeni.

Waziri Mkuu alijibu kuwa Naibu Spika akiitoa kauli kwa maamuzi ya kibunge itakuwa bora zaidi. Hata hivyo, Ndugai kakutoa kauli yoyote.

Lugora alitoa shutuma hizo wakati wa mjadala wa hotuba ya bajati ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakati mkutano wa bunge la sasa uliponza mjini Dodoma, na kutishia kwamba atawataja hadharani.

Mbunge huyo ni miongoni mwa wabunge ambao wamekuwa mwiba kwa serikali kutokana na kuipinga waziwazi na hata kutishia kuondoa shilingi katika bajeti za wizara ikiwamo ya Maji ambayo alitumia picha ya wanawake wanaosaka maji kuwataka wabunge wenzake waungane naye kuikataa bajeti hiyo.

Aliita picha hiyo kuwa ni sawa na nyoka wa shaba katika Bibilia aliyetengenezwa na Musa ili kuwaponya wana wa Israel.


 
CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment