‘Utapiamlo unaua watoto 130 kila siku’

WATOTO 130 walio chini ya umri wa miaka mitano, wanakufa kila siku nchini kutokana na utapiamlo unaotokana na lishe duni. Akizungumza Dar es Salaam juzi, Mkurugenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), Dk. Ali Mzige, alisema utapiamlo upo katika mikoa inayozalisha chakula na matunda kwa wingi.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Morogoro, Mbeya, Tanga, Rukwa, Iringa na Manyara.

Alisema tatizo jingine la utapiamlo ni kula chakula kupita kiasi kama vyakula vyenye wanga na sukari kwa wingi, mafuta kwa wingi na kuleta magonjwa yasiyoambukizwa kwa watoto na watu wazima.

Alisema sensa ya mwaka 2012, ilionyesha kuwa asilimia 42 ya watoto chini ya miaka mitano hapa nchini wamedumaa, asilimia 16 wana uzito pungufu na asilimia tano wamekonda wako katika rangi nyekundu ya kadi ya mtoto.

“Lishe bora na kamili huanzia nyumbani ni juu ya jamii kupata elimu wale chakula cha aina gani ambacho kitakuwa ni mlo kamili.

“Maziwa ya mama ni chakula tosha kwa miezi sita, bila kuongeza au kumpa mtoto maji asilimia 80 ya maziwa ya mama ni maji.

“Watoto wengi hupelekwa kwa waganga wa tiba asili na kukatwa kimeo, ninapenda kuwaeleza bayana Watanzania wenzangu waliopo mjini na vijijini kuwa hakuna ugonjwa wa kimeo na mtoto anapokonda kuna sababu lukuki mojawapo ni ugonjwa ambao hujitokeza kwa kukohoa au homa lakini sio kimeo hivyo msiwakate watoto vimeo wapelekeni hospitali,” alisema Dk. Mzige.

Alisema Hospitali ya IMTU kwa kushirikiana na Bango Sangho wamepanga kupima afya kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano bila malipo yoyote Mei 26, 2013 kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa nane mchana.

Alisema watapima uzito ambao takwimu zake ni kilogramu 10 kwa mtoto wa mwaka mmoja na nusu, kilogramu 12 kwa mtoto wa miaka miwili, kilogramu 13 kwa mtoto wa miaka miwili na nusu, kilogramu 14 kwa mtoto wa miaka mitatu.

Alisema kilogramu 15 kwa mtoto wa miaka mitatu na nusu, kilogramu 16 kwa mtoto wa miaka minne, kilogramu 17 kwa mtoto wa miaka minne na nusu na kilogramu 18 kwa mtoto wa miaka mitano.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment