Wafaransa wakiandamana kupinga ndoa za jinsi moja katika mji wa Lille, Desemba 8, 2012. |
Bunge la seneti nchini Ufaransa limeidhinisha muswada tata wa ndoa ya jinsia moja, licha ya upinzani mkubwa dhidi ya sheria hiyo.
Jana jumanne, bunge la juu la Ufaransa liliidhinisha muswada huo kwa kura 179 dhidi ya kura 157. Muswada huo unahalalisha na kuwaruhusu watu wa jinsia moja kuoana.
Sheria nyingine kuhusu wanandoa wa jinsia moja kuasili watoto itapigiwa kura wakati mwingine.
Ufaransa imeshuhudia maandamano makubwa dhidi ya muswada wa ndoa ya jinsia moja, yakiwemo yale ya tarehe 24 Machi, ambapo polisi waliwashambulia maelfu ya waandamanaji kwa mabomu ya kutoa machozi.
Bunge dogo la Ufaransa liliupitisha muswada huo mnamo Februari 12 kufuatia mjadala mzito uliodumu kwa saa 110.
Wapinzani wa muswada huo wanasema kuwa watoto wana haki ya asili ya kuwa na baba na mama na kwamba sheria hiyo itapelekea kuiharibu na kuidhalilisha taasisi ya familia.
Makanisa ya Ufaransa nayo pia yaliulaani muswada huo na kuiita ndoa ya mashoga “aibu” ambayo “itaitikisa misingi ya jamii yetu.”
Rais Francois Hollande aliahidi kuunga mkono muswada huo, kwa sababu hilo lilikuwa miongoni mwa ahadi zake wakati wa kampeni za kuwania urais wa nchi hiyo.
Mataifa mengine kadhaa ya Ulaya, kama vile Uholanzi, Ubelgiji, Denmark, Ureno, Norway, Uhispania, na Sweden zimeshaidhinisha ndoa ya jinsia moja.
0 comments:
Post a Comment