RIPOTI MAALUMU: UKAHABA WASHAMIRI



*Wanafunzi vyuoni, sekondari, shule za msingi wasagana, walawitiana, wajiuza
*Mawakala wa ngono wajichimbia kwenye vitongoji kadhaa jijini Dar es Salaam
*Wafanyabiashara, wananasiasa, vigogo wa Serikali ndiyo wateja wakubwa Dar, Dom


WAKATI chanzo cha ufaulu duni wa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012 ukiwa bado katika uchunguzi wa Serikali, uvundo mkubwa umebainika kwenye asasi, shule na vyuo mbalimbali nchini na kutishia ustawi wa jamii ya Kitanzania.

Utafiti uliofanywa kwa muda na RAI umebaini tishio kubwa kwa wazazi wa leo hasa baada ya kugundulika kwa vitendo vya vijana wa kiume wa shule za sekondari kujihusisha na ushoga, na mbaya zaidi kuwapo kwa watoto wa shule za msingi wanaolawitiana.

Vyuo vilivyomulikwa jijini Dar es Salaam ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwenye hosteli za Mlimani, Kijitonyama na Mabibo; Chuo cha Ustawi wa Jamii na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM)vilivyogeuka vyanzo vya idadi kubwa ya makahaba vijana wanaofurika mitaani, hasa maeneo ya Afrika Sana.

Vyuo vingine ni CBE cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na kile cha Mipango cha huko huko Dodoma.

“Lakini hawa unaowaona si wanafunzi wa vyuo tu, hapa wapo pia akina dada kutoka Shule ya Sekondari Makongo,” mmoja kati ya watu waliozungumza na RAI karibu na Klabu ya Usiku ya Ambiance aliliambia gazeti hili.

Taarifa ya kuwapo mabinti wa sekondari maeneo hayo usiku yalililazimisha RAI kubisha hodi kwenye Sekondari ya Makongo, ambako mmoja kati ya watu waliozungumza kwa sharti la kutotajwa gazetini alisema kuwa mbali na ukahaba huo, pia wapo mabinti wa shule hiyo ambao husagana huku vijana nao wakifanya vitendo vya ushoga.

Mkuu wa Shule ya Makongo, Luteni Kanali Selestine Mwangasi alikiri kuwapo kwa taarifa za wanafunzi wanaojihusisha na kusagana na ushoga, lakini akasema kuwa uchunguzi alioufanya ulishindwa kuthibitisha kashfa hizo.

“Suala la kusagana lilifika mezani kwangu kutoka kwa mzazi mmoja aliyelalamikiwa na binti yake. Nilipoanza kulishughulikia, yule mzazi na hata binti yake hawakutoa ushirikiano na kisha akamuhamisha shule mwanaye.

“Kukosekana kwa ushirikiano kulikwamisha uchunguzi wetu. Lakini hawa mabinti ni vyema kuwachunguza sana kwani wanaweza kuzusha jambo kumbe wamechoshwa na shule au uwezo wao darasani ni mdogo,” alisema.

Mkuu huyo wa Shule alikiri kumfahamu kijana mmoja anayedhaniwa kuwa ni shoga, lakini akasema kuwa uchunguzi wa kialimu na hata wa kijeshi haukufanikiwa kupata ushahidi wa kutosha.

Kwa upande wa vyuoni, wanafunzi kadhaa walikiri kujihusisha na ukahaba wengi wakiwa na lengo la kujiongezea kipato.

Mmoja aliliambia gazeti hili kuwa si wote wanaokwenda Ambiance au ‘viwanja’ vingine kujiuza, bali wapo wanaounganishiwa ‘dili’ na mawakala kadhaa jijini.

“Wapo mawakala wenye uwezo wa kukuunganisha na mtu au watu wenye fedha zao. Kwa mfano (anataja jina) wa Kinondoni. Huyu ni fresh (safi) kabisa kwani hana longolongo akikitafutia mteja,” alisema.

Mbali na wakala huyo wa Kinondoni, RAI liligundua mawakala wengine maarufu wanaoishi Mikocheni na Sinza jijini hapa ambao kazi kubwa inayowaingizia kipato ni kuwaunganisha wanafunzi na wanaume wakware ndani na nje ya Dar es Salaam.

Wateja wanaotajwa zaidi kupenda kuunganishiwa wanafunzi ni wafanyabiashara wa madini kutoka Kanda ya Ziwa, Mahenge na sehemu nyingine kadhaa nchini; wauza unga maarufu jijini, wabunge hasa wanapokuwa Dodoma na vigogo wakubwa serikalini wakiwa Dodoma kikazi na hata hapa hapa Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa uchunguzi wetu, mawakala hao magwiji kwa kuunganisha vigogo na mabinti wa vyuo vya elimu ya juu mara nyingi husafiri hadi Dodoma kwa ajili ya kazi hiyo hasa nyakati za vikao vya Bunge (kama sasa) na mikutano ya vyama hasa ile ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho wajumbe wake wengi ni vigogo serikalini na wafanyabiashara wakubwa.

Fedha zinazotozwa kwa kila ‘dili’ hazikuweza kufahamika mara moja kwani mabinti wengi hawakuwa tayari kulizungumzia hilo, lakini kwa mwonekano wa maisha ya mawakala hao, ni wazi hujipatia fedha za kutosha.

Siku kadhaa zilizopita, gazeti dada la hili, MTANZANIA liliandika makala ndefu ikizungumzia vitendo vya kulawitiana vinavyofanywa na watoto wa shule za msingi na sekondari jijini, likiweka wazi kuwa ifikapo mwaka 2020 Tanzania itakuwa na idadi kubwa ya mashoga, wanafunzi wenye Virusi vya Ukimwi na mateja.

Vitendo hivyo hufanyika maeneo ya shule, vituo vya mabasi yaendayo mikoani, daladala, vyumba vya masomo ya ziada (tuition) na katika baadhi ya vituo vya kulelea yatima. 

Miongoni mwa shule hizo ni Shule ya Msingi Mbuyuni iliyopo Oysterbay, Mchikichini, Shule ya Sekondari Binti Mussa, shule za msingi Kiwalani, Kigilagila, Hekima, Buguruni huku pia shule za Wailes, Sandali, Vetenari na Majani ya Chai zikitajwa.

Walimu kadhaa wa shule hizo walitupia lawama ushirikiano uliopo kati ya watoto wa shule hizo na majirani katika kushamiri kwa vitendo hivyo, hasa zile zilizozungukwa na makazi ya watu na biashara za chipsi, supu, pombe na vyakula vingine.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kiwalani, Fedes Shayo pamoja na Mwalimu Claudia Adamu anayesimamia Mradi wa Ukimwi na Ushauri chini ya ufadhili wa Serikali ya Ubeligiji, walikanusha kuwapo kwa vitendo hivyo shuleni hapo, ingawa Mwalimu Mkuu Msaidizi, Ilianola Bandola alitofautiana nao kidogo akisema zimewahi kufika taarifa za mwanafunzi wao aliyelawitiwa nje ya shule.

Mwalimu huyo alilaumu vibanda vya video vilivyopo mitaani vinavyoonyesha picha za ngono, wenyewe wakiziita ‘pilau’, akisema zinachangia kuwapo kwa maadili mabaya kwa watoto na vijana.

Mmoja wa wazazi aliyezungumza na RAI aliwalaumu mabinti wa sekondari na vyuoni kupendelea sana kutembelea mtandao wa kijamii wa Facebook akisema umekuwa chanzo cha mahusiano na wanaume wasiowajua na kujikuta wakiingia kwenye biashara haramu ya ngono.

CHANZO: Rai
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment