Kuku wakiuzwa mtaani mjini Shanghai, China, mnamo Aprili 1, 2013. |
Vifo kutokana na ugonjwa wa mafua ya ndege aina ya H7N9 vimeongezeka na kufikia 13 baada ya wagonjwa wengine wawili walioathiriwa na virusi hivyo kupoteza maisha yao nchini China.
Mpaka sasa, jumla ya watu 60 nchini humo wameathiriwa na mafua ya ndege aina ya H7N9.
China ilithibitisha rasmi kutokea kwa maambukizi ya virusi hivyo vipya vya mafua ya ndege wiki mbili zilizopita na mradi wa utafiti ulizinduliwa rasmi mnamo Aprili 10 kwa lengo la kutengeneza chanjo ya virusi hivyo.
Mradi huo unaofanywa kwa ushirikiano wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia na Tume ya Taifa ya Afya na Uzazi wa Mpango, unalenga kuzalisha chanjo ya virusi hivyo ndani ya miezi saba ijayo.
Hatua hiyo inakuja wakati Shirika la Afya Duniani likisema kuwa hakuna ushahidi kuwa virusi vya H7N9 vinaweza kusambaa miongoni mwa watu.
Shirika hilo lenye makao makuu mjini Geneva pia limetangaza mipango ya kutuma timu ya wataalamu wa kimataifa kwenda China kufanya utafiti juu ya virusi hivyo vipya vya mafua ya ndege.
H7N9 ni tofauti na virusi vya H5N1, ambavyo tangu mwaka 2003 vimesababisha zaidi ya vifo 360 vilivyothibitishwa na kuua makumi kwa mamilioni ya ndege.
0 comments:
Post a Comment