
Mfungwa mmojawa Kipalestina, aliyekuwa ameshikiliwa katika gereza la Waisraeli, ameripotiwa kfariki dunia na hivyo kuvuta hisia za ulimwengu juu ya hali za mateka hao walio katika jela za Wazayuni.
Vyanzo kutoka Chama cha wafungwa wa Kipalestina vinasema kuwa taarifa za kifo cha mfungwa huyo katika gereza la Magiddo zimetolewa leo Jumamosi. Hata hivyo, ripoti rasmi juu ya chanzo cha kifo chake haijatolewa.
Waziri katika mamlaka ya Palestina anayehusika na masuala ya wafungwa amemtaja mfungwa huyo kuwa ni Arafat Jaradat. Redio ya Israeli ilisema kuwa Mpalestina huyo mwenye umri wa miaka 30 alifariki kutokana na shinikizo la moyo.
Zaidi ya wafungwa 4,500 wa Kipalestina wanashikiliwa katika magereza mbalimbali ya Israeli, wengi wao bila kufunguliwa kesi au kupelekwa mahakamani. Wafungwa wanne kati yao -- Ayman Sharawneh, Samer al-Issawi, Jaafar Ezzedine, na Tareq Qaa’dan –wamekuwa katika mgomo wa muda mrefu wa kukataa kula.
Hali mbaya ya kiafya ya wafungwa hao wanne imeibua maandamano makubwa katika maeneo ya Wapalestina. Walipelekwa hospitali siku ya Ijumaa.
Wanne hao wamekuwa kwenye mgomo wa chakula kwa miezi kadhaa sasa wakipinga kuwekwa kizuizini, kitendo chenye utata kinachofanywa na Tel Aviv, ambacho huiruhusi mamlaka ya Israeli kuwashikilia Wapalestina bila kuwafungulia mashitaka.
Issawi alikamatwa Julai 2012 miezi kadhaa tu baada ya kuachiwa huru kama sehemu ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa baina ya Israel na Hamas.
Mnamo Februari 21, Issawi, 33, alipewa adhabu ya miezi 8 jela kwa kukiuka masharti ya kuachiwa huru katika kifungo cha awali.
0 comments:
Post a Comment