BUNGE LA UINGEREZA LAIDHINISHA NDOA ZA JINSIA MOJA



Bunge la Uingereza limeidhinisha ndoa za jinsia moja licha ya upinzani mkali kutoka kwa wabunge wa chama cha Conservative cha Waziri Mkuu David Cameron.

Siku ya Jumanne, wabunge hao waliidhinisha muswada wa sheria inayoruhusu ndoa za jinsia moja kwa kura 400 dhidi ya 175.

Hatua hiyo inaifanya Uingereza kuungana na nchi kumi zinazoruhusu watu wa jinsia moja kuoana, lakini Cameron alikuwa na wakati mgumu sana kuwaona wabunge wa chama chake wakikataa kumuunga mkono.

Ni wabunge 127 tu kati ya 303 wa chama chake cha Conservative ndio waliopiga kura kuunga mkono mpango huo, huku 136 wakipiga kura kuukataa na wengine 40 wakijizuia kupiga kura.
"Mtazamo mkali upo kwa pande zote mbili lakini ninaamini wabunge kupiga kura inayowawezesha mashoga kuoana  ni hatua moja mbele kwa ajili ya nchi yetu,” aliandika Cameron kwenye ukurasa wake wa Twitter baada ya upigaji huo wa kura.

Muswada huo ulioandaliwa na serikali utawawezesha mashoga kuoana kwa taratibu za kiraia na za kidini, iwapo taasisi za kidini zitaridhia.

Matokeo hayo yalikaribishwa vyema na washirika wa Cameron katika serikali, yaani chama cha Liberal Democrats, na pia kambi ya upinzani ya chama cha Labour, huku kundi la utetezi wa haki za mashoga la Stonewall likiyaita matokeo hayo kuwa ni “hatua ya kweli ya kihitoria".

Naibu Waziri Mkuu Nick Clegg, ambaye ni kiongozi wa chama cha Liberal Democrats, aliyaelezea matokeo hayo kuwa ni "msingi wa alama ya usawa".

"Kura ya leo inaonesha kuwa bunge linaunga mkono kwa nguvu zote usawa katika ndoa,” alisema na kuongeza: “Ndoa ni upendo na uamuzi, na watu hawatakiwi kunyimwa ndoa kwa sababu tu wao ni mashoga.”

Kwa sasa, wanando wa jinsia moja wana uhuru wa kuungana, ambapo watapata haki na ulinzi wote wa kisheria katika masuala kadhaa wa kadhaa kama vile mirathi, pensheni, na huduma za mtoto.

'NI KINYUME NA MAADILI'

Wakati wa mjadala uliodumu kwa zaidi ya masaa sita, wabunge wengi wa chama cha Conservative waliilaani sheria hiyo, wakisema kuwa inakwenda kinyume na maadili, sio kipaumbele cha taifa, na inatsababisha mkanganyiko usio wa lazima.

Mbunge wa chama cha Conservative, Gerald Howarth aliliambia bunge kuwa serikali haikuwa na mamlaka ya kufanya “mabadiliko makubwa ya kijamii na kiutamaduni.”

Waziri wa Utamaduni Maria Miller, ambaye ndiye anayeshusika na sheria hiyo, alisisitiza kuwa muswada huo utalinda uhuru wa dini na “hautawanyanyapaa wale wanaoamini kuwa ndoa inatakiwa kuwa kati ya mwanaume na mwanamke”.

Kanisa la Anglikana, ambayo ndiyo dini rasmi ya nchi hiyo, halijahusishwa katika ufungishaji wa ndoa hizo.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa Kanisa hilo, ambalo linapinga ndoa za mashoga, linalindwa kisheria dhidi ya madai kwamba kama dini rasmi ya nchi linapaswa kumfungishia ndoa kila anayeomba kufanyiwa hivyo.

Muswada huo unatakiwa kuchunguzwa na kamati ya wabunge kisha upelekwe mbele ya Bunge kubwa kabla ya kuwa sheria rasmi.

Wakati watu wengi nchini Uingereza wanaunga mkono ndoa za jinsia moja, maoni yanaonesha kuwa hatua ya Cameron ya kuunga mkono suala hilo inaweza kukinyima chama chake nafasi ya kushinda katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment