
Wakazi wawili katika Kijiji cha Karungu, Kata ya Ivuna, wilayani Momba, katika Mkoa wa Mbeya wamefariki dunia baada ya kufukiwa wakiwa hai katika kaburi moja na marehemu waliodaiwa kusababisha kifo chake kwa njia za kishirikina.
Kwa mujibu wa Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ivuna, Joseph Silwimba, Marehemu Nongwa Hussein ambaye alidaiwa kuuawa na watu hao alifariki dunia Jumamosi iliyopita baada ya kuugua kwa muda mrefu, lakini baadhi ya wakazi wa kijiji hicho cha Karungu walihusisha ugonjwa huo uliosababisha kifo chake na ushirikina.
Kaimu mtendaji huyo alieleza kuwa tukio hilo la kinyama lilitokea siku hiyo mchana, muda mfupi baada ya jeneza la marehemu Hussein kuingizwa kaburini. Alisema kabla ya kufukiwa katika kaburi moja na marehemu Hussein watu hao, Ernest Molela na Bibi Mizinala Nachela walipigwa hadi kuzirai na baadaye kusukumizwa katika kaburi alimokuwa marehemu Hussein. Hivyo, marehemu Hussein alizikwa bila kufanyiwa ibada.
Hicho hakika ni kisa cha ajabu ambacho ni vigumu kuingia akilini na ndiyo maana tumesema hapo juu kwamba kisa hicho kinasikitisha na kutonesha vidonda.
Tunasema ni kisa kinachotonesha vidonda kwa kuwa wilaya hiyo ya Momba ilianzishwa majuzi tu na Serikali kutoka katika Wilaya ya Mbozi ambayo miaka michache iliyopita ilivuma nchi nzima kwa vitendo vya kinyama vya uchunaji wa ngozi za binadamu kutokana na imani za kishirikina kwamba ngozi ya binadamu inaleta utajiri wa haraka.
Ni tukio linalotonesha vidonda vya Watanzania kutokana na vitendo kama hivyo vilivyotokea katika sehemu mbalimbali hapa nchini huko nyuma kutokana na imani za kishirikina. Nani hakumbuki mauaji yaliyotikisa nchi nzima ya watu wenye ulemavu wa ngozi, yaani albino, ambao waliuawa kinyama au sehemu za miili yao zilikatwa na kuuzwa kwa fedha nyingi kwa imani za kishirikina kwamba viungo vya watu hao vinaleta utajiri wa ajabu?
Watanzania hatujasahau vitendo vingine vya kinyama waliotendewa wananchi wenzetu katika sehemu mbalimbali nchini kwa sababu za imani za kishirikina. Hatujasahau mauaji ya kuua watu kwa nondo mkoani Mbeya kwa imani hizo na pia hatujasahau mauaji ya watu wenye vipara mkoani Kigoma kwa sababu hizo za kishirikina kwa lengo la kupata utajiri.
Hoja yetu hapa ni kwamba ushirikina ni hatari na adui mkubwa wa maendeleo ya binadamu.
Hoja yetu hapa ni kwamba ushirikina ni hatari na adui mkubwa wa maendeleo ya binadamu.
Utafiti umeonyesha bayana kwamba maeneo ya watu wanaoendekeza imani za ushirikina hapa nchini hayakaliki, kwa maana ya wakazi wake wengi kuondoka na kukimbilia mijini na kuishi huko maisha yao yote. Ni vitendo vya kishirikina vinavyowakwaza watu kupata elimu au kujenga nyumba nzuri na kuishi maisha mazuri huko vijijini hata kama wana uwezo wa kufanya hivyo. Ni vitendo hivyo na imani hizo ndizo zinazowakwaza watumishi wa umma kufanya kazi katika baadhi ya maeneo hapa nchini.
Sisi tunasema vitendo na imani hizo lazima vikomeshwe ikiwa tunataka kusonga mbele kimaendeleo kama taifa. Serikali ionyeshe njia, kwa mfano, kwa kuweka mikakati ya kudhibiti kazi za waganga wa kienyeji na kuelimisha umma kuhusu madhara ya imani za kishirikina.
Vinginevyo, wananchi watazidi kupoteza maisha kama tulivyoona katika tukio la juzi katika Mkoa wa Mbeya na matukio mengine ya aina hiyo katika sehemu nyingine nchini katika siku za nyuma.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment