UBAKAJI WA KUTISHA KATIKA MAKAMBI YA MOGADISHU

Nyumba nyingi katika makambi ya ndani hazina usalama


Baada ya mgogoro wa muda mrefu uliodumu kwa zaidi ya miongo miwili, sasa kuna aina fulani utulivu na usalama nchini Somalia. Watu waliokuwa wakilinda mitaa wakiwa wamefunika nyuso zao wameondoka na badala yake wapo watu waliovalia sare ambazo kwa nje zinaonekana kama sare maridadi.

 Vizuizi vya barabarani vilivyokuwa vikiugawa mji kati ya eneo linalotawaliwa na serikali na linalotawaliwa na wapiganaji wa al-Shabab vimeondolewa; magari yanapita bila kuzuiliwa. Wasomali wanamiminika kwenye fukwe za bahari, nyumba kongwe zinakarabatiwa na nyumba mpya zinajengwa.

Lakini sio watu wote wanaofurahia aina hii ya usalama.

Makambi yaliyojaa wakimbizi wa ndani, waliolazimishwa kuyakimbia makazi yao kutokana na vita na ukosefu wa usalama, bado yanashuhudiwa. Lakini kwa wanawake wanaoishi katika makambi hayo, ukosefu wa amani na usalama limekuwa jambo nyeti sana.


Nura Hirsi, mjane mwenye umri wa miaka 27 anayeishi katika kambi ya Burdubo katika eneo la Tarabunka magharibi mwa Mogadishu. Anasema kuwa alibakwa na wanajeshi saba wa serikali walipovamia makazi yake siku ya Jumamosi, Desemba 29.

"Ilikuwa saa 7 usiku, watoto walikuwa wamelala, ndipo wanaume hawa walipoingia. Baadhi yao walikuwa na silaha aina ya AK47. Walinipiga makofi, wakanimuru kutoka nje na kunibaka. Sikuweza kupambana nao wala kujitetea. Ningewezaje kupambana na watu wenye silaha?"

Nura anasema kuwa hakuna mtu ambaye angekuja kumnusuru wakati akishambuliwa.

"Watu wanaogopa kutoka ndani usiku kuja kuangalia kinachotokea. Kila mtu anaogopa; wanahofia maisha yao.

"Baada ya kuondoka, nililia sana. Asubuhi nilikwenda hospitali wakanipa dawa fulani ya kumeza, lakini sikuwaambia yaliyotokea usiku. Ni Wasomali na hawataki kujua."

Mamlaka hazichukulii kwa uzito tuhuma za ubakaji, hata ule unaofanywa na makundi ya wahuni, alisema.

"Nilikwenda polisi lakini hawakulipa uzito. Watu wanauawa Mogadishu; lakini mimi sikufa. Kwao ubakaji sio jambo zito. Hata kiongozi wa kambi halitilii maanani. Nilipomwambia hakusema chochote. Nilitamani hata kuongea na vituo vya redio-lakini nani atakayekupa nafasi hiyo?"

UNYANYAPAA

Abdalle Muumin ni mwandishi wa habari wa Kisomali. Anasema kuwa vyombo vya habari vya nchi hiyo vinapuuzia masuala ya dhulma za ngono, jambo linalopelekea waathrika wa ubakaji kunyanyapaliwa.

"Kuna utamaduni fulani hapa Somalia, ambapo muathirika wa vitendo vya ubakaji ataripoti kuwa kuna mtu fulani alijaribu kunibaka, lakini hakuna mtu atakayejitokeza akazungumza na kusema kuwa mtu fulani alibakwa," alisema Abdalle.

"Sababu nyingine inayofanya usisikie chochote kuhusu habari zinazoyahusu makambi ya ndani ni kwa kuwa wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari hawajali na hawazipi umuhimu wowote. Waandishi wanapopeleka habari zinazohusu makambi ya ndani hazitangazwi; wanaziita kuwa ni shuban biyood ["uharo"].

"Wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari wanazipa umuhimu habari za kisiasa; ni gharama kuendesha redio. Katika siasa kuna pesa."

Fartun Abdisalaan Adan ni mwanzilishi mwenza wa taasisi ya Sister Somalia, iliyoanzsihwa mwaka 2010 na kufungua kituo cha kwanza mjini Mogadishu kushughulikia migogoro ya ubakaji.

Mwelekeo wa ubakaji unabadilika kidogo kidogo, alisema. Attitudes towards rape are slowly changing, she said. Suala hili sio mwiko tena - lakini zinahitajika juhudi za ziada kukabiliana nalo: "Tulipoanza kazi zetu, tulikabiliana na vikwazo vikubwa kutoka serikalini na kutoka kwa wanaume pia, na wanawake wengi waliona aibu kulizungumzia- lakini hatua kwa hatua walituamini. Sasa watu nchini Somalia wanalizungumzia, hakuna anayekataa kuwa halitokei, ingawa mwitikio bado uko chini."

Hata hivyo, ubakaji bado ni tatizo kubwa, na waathrika wapya saba hufika kila wiki kwenye ofisi za kituo cha  Sister Somalia mjini Mogadishu.

"Wanawake katika makambi ya ndani wanaishi katika mazingira magumu mno. Ukiangalia wanaoishi katika  makambi hayo, utakuta wengi wao ni wanawake wajane wenye watoto. Kambi hiyo sio nyumba, hakuna mlango. Mwanaume anaweza kuja muda wowote na kufanya chochote anachotaka, akijua kuwa hakuna shida itakayomkuta.

Waathirika wa ubakaji wanapokuja ofisini kwetu, jambo la kwanza tunawapeleka hospitali kupata msaada wa tiba na kulipia gharama za matibabu; kisha sasa tunarudi kituoni ambapo ushauri nasaha huanza. Vilevile tunajadiliana nao kujua kama wanataka kurudi nyumbani kwao. Wakiamua kuondoka basi tunawasaidia kwa kuwapeleka sehemu nyingine. Vilevile tumeanzisha nyumba maalumu yenye usalama ambapo wanaweza kukaa kwa muda kabla ya kupata makazi yanayofaa. Kwa sasa tunawasaidia wanawake 400 ambao wamebakwa au ambao mabinti zao wamebakwa," alisema.

Nyumba hiyo inawafaa zaidi mabinti ambao wamezikimbia familia zao baada ya kupata ujauzito kutokana na kubakwa.

"Mabinti wadogo, wenye umri kati ya 16 au 17, huwa wanaogopa kuwaambia wazazi wao kwamba wamebakwa na kuwa kuna uwezekano wakawa na mimba, kwa hofu kwamba hawataaminika, hususan na baba zao; hivyo wanakimbia na kukaa katika kituo chetu. Mabinti hawa  ndio wanaosita kusema kuwa walibakwa kwa sababu wanahofia mustakbali wao na kwamba kuwa muathrika wa ubakaji kutawapunguzia nafasi ya kuolewa.'

'SIO SUALA LA WANAWAKE'

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Galcayo, kusini kati mwa Somalia, mwanaharakati wa huduma za kibinaadamu na mshindi wa mwaka huu wa tuzo ya Nansen Refugee Award, Hawa Aden Mohammed, alielezea wasiwasi wake kuhusu utamaduni wa waathirika kutozunguzia matukio ya kubakwa.

"Sio rahisi kuchukua hatua ya kisheria katika hali ambayo sheria imekomeshwa au haipo. Kwa uzoefu wangu, asilimia 90 ya wale waliobakwa wanashindwa kwenda kwenye mamlaka husika kwa sababu wanaogopa au hawaamini kuwa kuna hatua inayoweza kuchukuliwa. Vilevile kuna haja ya kutoa elimu; wengi katika wanawake hawa wanaona aibu, wanajiona kama watu duni na hawataki kulizungumzia.

Vilevile serikali inahitaji kulizungumzia suala hili la ubakaji. Hili sio suala la wanwake, ni suala la jamii."

Serikali mpya ya Somalia imeingia madarakani miezi miwili tu iliyopita, lakini kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Kazi, Vijana na Michezo, Aweis Haddad, "serikali inafanya juhudi kubwa kuzuia mambo kama hayo. Mojawapo ya mambo yaliyofanywa na rais alipoingia madarakani ni kuzunguzia dhulma ya ubakaji na dhulma nyingine za kijinsia."

Alihitimisha kwa kuhamisha lawama, akakanusha taarifa ya wanajeshi wa serikali kuhusika na dhulma ya kingono dhidi ya wanawake kama Nura mwenye umri wa miaka 27.

"Watu wengi wanaweza kuvaa sare za serikali na kujifanya kuwa ni polisi au wanajeshi, lakini sio. Hivyo hivyo hata kwa upande wa Shabab," alisema.

"Kila uhalifu tunaushughulika kwa uzito. Mtu yeyote katika serikali akigundulika kuwa nyuma ya vitu hivyo, hatua itachukuliwa dhidi yake."


IMEANDALIWA NA KABUGA KWA HISANI YA MASHIRIKA YA HABARI!
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment