![]() |
| Rais Armando Guebuza wa Msumbiji |
MADAKTARI nchini Msumbiji wamefanya mgomo wakidai kupandishwa kwa mishahara na maboresho ya mazingira ya kazi, ambayo wanadai hayajatekelezwa na serikali. Katika kuonesha dhamira yao, leo Jumatatu, Madaktari hao waliipuuza serikali ambayo ilipiga marufuku wa umma kufanya mgomo. Haijawa wazi ni madaktari wangapi wamehusika katika mgomo. Lakini hali katika hospitali kuu katika mji mkuu Maputo, inaelezwa kuwa ya kawaida licha ya mgomo huo. Imeelezwa kuwa kweli madaktari wamefanya mgomo, lakini wamekuwa wakitoa huduma za msingi. Mapema, rais wa Jumuiya ya Madaktari, Jorge Arroz, alisema: "Kuanzia Jumatatu, terehe 7 Januari, madaktari wote nchini Msumbiji watadumaza shughuli zao kwa kuwa serikali imeshindwa kushughulisha madai yao kuhusu mishahara, malazi na haki za madaktari." Jana Jumapili, wizara ya afya ilisema kuwa hakuna sheria nchini Msumbiji inayowaruhusu wafanyakazi wa huduma muhimu za umma kufanya mgomo. Mwezi uliopita, vyombo vya habari vya nchi hiyo viliripoti kuwa madaktari walikuwa wakidai mshahara wa awali wa dola 600 na 1,200. Vilevile madaktari hao wanataka kuwa na haki sawa ya kuishi katika nyumba za serikali, ambazo wanadai kuwa zinatolewa kwa kuwapendelea madaktari wa kigeni. Awali mgomo huo ulikuwa umetangazwa kufanyika mwezi Desemba ya mwaka uliopita, lakini ukaakhirishwa kwa sababu ya mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina ya madaktari na serikali. Kwa mujibu wa tovuti ya All Africa, siku ya Ijumaa, waziri wa Afya, Alexandre Manguele, alisema kuwa serikali haina fedha za kulipa ongezeko hilo la mishahara kwa kiwango kinachodaiwa na madaktari. Msumbiji ina jumla ya madaktari 1,200 katika hospitali za umma na zile za binafsi nchi nzima, huku kukiwa na uuwiano wa daktari mmoja kuwahudumia watu 22,000. CHANZO: AL-JAZEERAH NA MASHIRIKAMBALIMBALI YA HABARI. |

0 comments:
Post a Comment