Mamia ya watu wanaishi katika makaburi ya Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Manispaa ya Kinshasa inasema imeshindwa kuwachukulia hatua watu hao ambao wamegeuza makaburi kuwa makaazi yao.
Taarifa zinasema familia karibu 100 wakiwemo watoto 500 walio chini ya umri wa miaka 10 wanaishi katika makaburi ya Kinsuka mjini Kinshasa.
Waziri wa Nyumba na Ustawi wa Miji katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Fridolin Kasweshi amesema nyumba za kuishi zilianza kujengwa katika makaburi hayo mwaka 2010 pamoja na kuwa serikali imepiga marufuku ujenzi huo.
Mwezi Aprili mwaka huu nyumba zilizojengwa makaburini mjini Kinshasa zilibomolewa kwa amri ya mkuu wa mkoa lakini usiku wa manane wakaazi walirejea na kujenga upya nyumba zao.
Waliojenga nyumba hizo katika makaburi mjini Kinshasa wanasema hawawezi kumudu kulipa kodi kutokana na mishahara duni.
Wataalamu wa afya wanasema wanaoishi makaburini hapo hasa watoto wanahatarisha afya zao.
0 comments:
Post a Comment