![]() |
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Francois Bozize |
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ameiomba Ufaransa na madola mengine ya nje kuharakisha kuisadia serikali yake kupambana na waasi ambao wameendelea kuiteka miji mbalimbali na kuukaribia mji mkuu.
Akizungumza na umati wa watu katika mji wa Bangui, mji wenye wakazi wapatao 600,000, jana Rais Francois Bozize aliyaomba madola ya nje kufanya kila linalowezekana. Aliitaja moja kwa moja Ufaransa, ambayo ni mkoloni wa zamani wa nchi hiyo.
“Ufaransa ina uwezo wa kuwazuia (waasi) lakini kwa bahati mbaya hawajatusaidia chochote mpaka sasa," alisema Rais Bozize.
Lakini Ufaransa ilikataa kutoa msaada wa kijeshi. Jana, Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, alisema kuwa nchi yake inataka kulinda maslahi yake huko Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini sio kuilinda serikali ya Bzize.
Matamshi hayo yanakuja siku moja baada ya mamia ya waandamanaji, waliochukizwa na kukosa msaada dhidi ya waasi, kuupiga kwa mawe Ubalozi wa Ufaransa mjini Bangui na kuondoka na bendera ya Ufaransa.
Wizara ya ulinzi ya Ufaransa inasema kuwa karibu askari 200 wa Ufaransa tayari wapo nchini humo, wakitoa msaada wa kiufundi na mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo.
Ufaransa inataka yafanyike mazungumzo ya amani baina ya serikali na waasi, huku wizara ya mambo ya nje ikisema kuwa mazungumzo hayo "yataanza hivi karibuni mjini Libreville (Gabon)".

WAGENI KUONDOKA
Wakati huo huo, Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, alizungumza kwa simu na Bozize, akimtaka Rais huyo kuchukua jukumu la kuhakikisha usalama wa raia na wanadiplomasia wa Ufaransa walioko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Jana, maafisa wa Marekani walisema kuwa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo, ilikuwa mbioni kufunga ubalozi wake na kuwaamuru wanadiplomasia wake kuondoka.
Maafisa hao walisema kuwa, balozi wa marekani na watu wengine wapatao 40, wakiwemo wamarekani kadhaa, waliondoka mjini Bangui kuelekea Kenya.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa waraka likielezea wasiwasi wake kuhusu hali inayoendelea nchini humo na kulaani mapigano hayo.
Mapema, serikali ya Bozize iliimtaka mshirika wake wa muda mrefu, Chad, kutuma askari 2,000 kuyapa nguvu majeshi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Lakini hapakuwa na uhakika iwapo askari hao wa Chad walikuwa wamewasili, na hata kama wangewasili, hakuna uhakika kama muungano wa majeshi hayo ungeweza kuhimili mashambulizi ya waasi.
Kwa uchache makundi manne tofauti ya waasi wanahusika katika haya mapigano, ingawa idadi yao kamili haijaweza kuthibitishwa.
'KIU YA HAKI'
Jamhuri ya Afrika ya Kati, taifa lenye watu milioni 4.4, imeathirika na miongo mingi ya mapinduzi ya kijeshi na uasi mbalimbali tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1960, na imeendelea kuwa miongoni mwa nchi maskini zaidi ulimwenguni.
Mwaka 2007 waasi hawa walisaini mkataba wa amani uliowawezesha kujumuishwa katika jeshi la nchi, lakini viongozi wa wapiganaji hao wanadai kuwa makubaliano hayo hayakutekelezwa kikamilifu.
Mpaka sasa, waasi wamekwishaiteka miji 10 yenye wakazi wengi kaskazini mwa nchi, na wakazi wa mji mkuu wana wasiwasi kuwa waasi hao wanaweza kuushambulia muda wowote, licha ya viongozi wa waasi kutoa hakikisho kwamba wako tayari kufanya mazungumzo badala ya kuushambulia mji wa Bangui.
Waasi hao wanadai kuwa hatua yao hiyo inalenga "kupatikana kwa haki, amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi ya watu wa Jamhuri ya Afrika ya kati."
0 comments:
Post a Comment