Siku ya Ijumaa Baraza la Kitaifa la Syria, ambalo ndio taasisi kuu ya upinzani nje ya nchi katika mapambano yanayoendelea dhidi ya Rais Bashar al-Assad, liimchagua mwanaharakati wa zamani George Sabra kuwa kiongozi wa Baraza hilo.
Sabra, ambaye ini Mkristo, anachukua uongozi wa baraza hilo ambalo limekuwa likikosolewa sana na washirika wake wa kimataifa kwa kutokuwa madhubuti katika mapambano dhidi ya serikali ya Syria na kwa kukumbwa na migogoro binafsi.
Mara tu baada ya kuteuliwa, Sabra aliomba silaha kwa ajili ya kupambana na majeshi ya Rais Assad. "Tunahitaji kitu kimoja tu ili kusaidia haki yetu ya kuishi na kujilinda: tunahitaji silaha, tunahitaji silaha," aliwaaambia waandishi wa habari baada ya kuteuliwa na baraza la utendaji la SNC lililokutana wiki hii nchini Qatar.
Siku ya Jumamosi, SNC itaanza mazungumzo na makundi mengine ya Syria ikiwa ni pamoja na wawakilishi wa makundi ya waasi yaliyo ndani ya Syria, ili kutengeneza taasisi mpya na pana kwa matarajio kutambuliwa na jamii ya kimataifa kama Serikali ya baadaye.
Qatar, Marekani na Dola nyingine zinayashinikiza makundi ya upinzani nchini Syria kuungana.
Qatar imewakaribisha mamia ya vigogo wa SNC na makundi mengine wiki moja iliyopita katika hoteli zenye hadhi ya nyota tano, huku wanadiplomasia wa Marekani wakishiriki ili kuwashinikiza kufikia makubaliano. Hata hivyo, SNC ina wasiwasi kuwa huenda ushawishi huo utakuwa na taathira katika muungano mpya.
Sabra alimshinda mgombea mwingine ili kumrithi Abdulbaset Sieda, Mkurdi anayeishi nchini Sweden, ambaye naye alipokea kijiti cha uongozi kutoka kwa kiongozi wa kwanza wa SNC, Burhan Ghalioun.
Mwanachama wa Muslim Brotherhood, Mohammed Farooq Taifoor alichaguliwa kuwa makamu wa Sabra. Vuguvugu la Muslim Brotherhood, ambalo lina ushawishi katika ulimwengu wa Kiarabu, linaonekana kuwa na sauti kubwa ndani ya Baraza hilo la SNC.
Sabra alisema kuwa kuteuliwa kwake kumeonesha kwamba hakuna udini ndani ya SNC. "Watu waliopo hapa ni Waislamu na wamemchagua Mkristo," alisema.
Sabra anatoka katika kitongoji cha Qatana kilicho mjini Damascus na kushiriki katika maandamano ya mwanzo dhidi ya Rais Assad mwaka mmoja uliopita, kabla ya kuikimbia nchi baada ya Polisi wa siri kuanza kuwalenga wale waliokuwa wakichochea maandamano.
Sabra mwenye umri wa miaka 65, ambaye ni mwalimu wa Jiografia, alikuwa mkosoaji mkubwa dhidi ya Rais Assad kabla ya kuanza kwa machafuko. Ni mtu aliye karibu na Riad al-Turk, mpinzani maarufu wa serikali anayeendesha harakati zake chini kwa chini huko Syria.
REUTERS.

0 comments:
Post a Comment