CRISTIANO RONALDO ATOA MSAADA WA €1.5 MILIONI KWA WATOTO WA GAZA
Mshambuliaji nyota wa timu ya soka ya Real Madrid ya Uhispania, Cristiano Ronaldo, ametoa msaada wa kitita cha €1.5 millioni kwa watoto wa Kipalestina huko Gaza. Taarifa hiyo imeandikwa katika mtandao wa klabu hiyo wa lugha ya Kiarabu.
Mshambuliaji huyo nyota alitoa Kiatu chake cha Dhahabu alichokipata mwaka 2011 kwa Taasisi ya Real Madrid. Taasisi hiyo ilikiuza kiatu hicho katika mnada na sasa itatoa pesa hizo kama msaada kwa ajili ya shule mbalimbali mjini Gaza.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, Taasisi ya Real Madrid Foundation imesaidia kujenga shule 167 katika nchi 66.
Sio mara ya kwanza kwa Ronaldo kutoa msaada. Mwaka jana aliuza viatu vyake vingi vya michezo katika mnada wa Taasisi ya Real Madrid ambavyo vilitolewa msaada kwa shule mbalimbali mjini Gaza.
Ronaldo alikuwa mchezaji ghali zaidi katika historia baada ya kuhama kutoka klabu ya Manchester United kwenda Real Madrid kwa uhamisho wenye thamani ya €93.9 millioni. Aidha, mkataba wake na Real Madrid, ambao analipwa €12 millioni kwa mwaka, unamfanya kuwa mongoni mwa wanasoka wanaolipwa fedha nyingi zaidi ulimwenguni.

0 comments:
Post a Comment