Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana lilipasisha azimio likilaani utumiaji wa aina yoyote wa watoto wadogo kama askari katika maeneo ya vita.
Azimio hilo pia limelaani vikali mashambulizi ya aina yoyote dhidi ya hospitali na vitendo vya kuzuia misaada ya kibinadamu kwa watu walioathiriwa na vita hususan watoto wadogo.
Wananchama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameeleza wasiwasi wao kuhusu vitendo vya kutumiwa watoto kama wapiganaji vitani na kutumiwa katika masuala ya ngono kunakofanywa na makundi ya waasi katika nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wametaka kupasishwa sheria kali za kimataifa za kukabiliana na uhalifu huo.
Hata hivyo baadhi ya nchi wanachama wa Baraza la Usalama hazikupigia kura azimio hilo na zimeukosoa Umoja wa Mataifa kwa kuwa na misimamo ya kinduma kuwili katika masuala hayo.
Nchi hizo zimeashiria mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la Marekani Machi mwaka huu katika kijiji kimoja huko Afghanistan ambapo wanakijiji 15 wakiwemo watoto 9 ambao hawakuwa na silaha wala hatia waliuawa kinyama. Mwakilishi wa wakati huo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Watoto Wadogo na Mapigano ya Silaha Radhika Coomaraswamy alikataa kusema lolote katika Baraza la Usalama au mahala pengine kuhusu mauaji hayo ya watoto wadogo yaliyofanywa na jeshi la Marekani huko Afghanistan.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)

0 comments:
Post a Comment