Emmanuel Niyonkuru, 54, waziri wa maji, mazingira na mipango, aliuawa usiku wa manane. |
Waziri wa mazingira nchini Burundi ameuawa usiku wa
Jumapili, polisi wamesema. Mauaji hayo ni ya kwanza ya aina yake tangu nchi
hiyo ilipotumbukia katika ghasia za kisiasa mwaka 2015.
Emmanuel Niyonkuru, mwenye umri wa miaka 54, ambaye
alikuwa waziri wa maji, mazingira na mipango aliuawa usiku wa manane, kwa
mujibu wa ujumbe uliotumwa kwenye mtandano wa Twitter na msemaji wa polisi Pierre
Nkurikiye.
Mauaji hayo ambayo ni ya kwanza dhidi ya waziri
anayehudumu katika serikali tangu Burundi ilipotumbukia katika mzozo wa kisiasa
kufuatia uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu mwaka 2015, yamekuja
baada ya miezi kadhaa ya utulivu.
"Waziri wa maji na mazingira ameuawa na mhalifu
mwenye silaha wakati akielekea nyumbani kwake Rohero, kwenye saa 6:45 usiku,"
Nkurikiye aliandika zikiwa zimepita saa nne baada ya tukio hilo.
Aliongeza kuwa mwanamke mmoja amekamatwa kufuatia “mauaji”
hayo.
Aidha, kwenye mtandao wa Twitter, Rais Nkurunziza alitoa
salamu za rambirambi kwa “familia na Warundi wote" akiapa kuwa uhalifu huo
utachukuliwa hatua.
Kwa uchache watu 500 wameuawa na wengine 300,000 wameikimbia
nchi hiyo tangu ghasia zilipozuka mwezi Aprili mwaka 2015.
CHANZO: Daily Monitor
0 comments:
Post a Comment