Mshambuliaji aliyevalia vazi la Krismasi maarufu kama
Santa Claus alifyatua risasi kwenye ukumbi mmoja wa usiku mjini Istanbul wakati
wa sherehe za kuukaribisha Mwaka Mpya.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Süleyman
Soylu, shambulizi hilo limewaua watu 39 na kuwajeruhi wengine 69.
Soylu amesema kuwa watu 16 miongoni mwa waliouawa
walitambuliwa kuwa raia wa kigeni, huku 5 wakiwa raia wa Uturuki. Juhudi zinaendelea
kuwatambua miili ya watu wengine 18. Aidha, waziri huyo ameeleza kuwa majeruhi
69 wako hospitalini wakipatiwa matibabu.
“Majeruhi 4 wako katika hali mbaya. Mmoja amejeruhiwa
vibaya sana,” amesema Soylu.
Afisa mmoja wa serikali ni miongoni mwa waliouawa katika
shambulizi hilo lililoulenga ukumbi wa Reina unaopatikana katika kitongoji cha Ortaköy
mjini Istanbul. Duru zinasema kuna uwezekano kwamba kulikuwa na washambuliaji
zaidi ya mmoja waliohusika katika shambulizi hilo. Wakati wa shambulizi hilo
zaidi ya watu 500 walikuwa ndani ya ukumbi huo.
Mshambuliaji alianza kuwafyatulia risasi polisi
waliokuwa nje ya ukumbi kabla ya kuingia na kuwafyatulia watu waliokuwa ndani. Baadhi
ya wateja walijirusha kwenye maji katika mkondo wa Bosporus ili kujinusuru na
shambulizi hilo.
Polisi wameanzisha msako mkubwa kumsaka mshambuliaji
huyo ambaye alifanikiwa kukimbia baada ya kufanya tukio hilo.
Hatua za kiusalama zimeimarishwa katika miji mikubwa
nchini Uturuki huku polisi wakiweka vizuizi kwenye maeneo muhimu ya kuelekea
katika miji ya Istanbul na Ankara.
Miji ya Ankara na Istanbul ililengwa na mshambulizi
kadhaa kwa mwaka 2016 yaliyotekelezwa na wapiganaji wa makundi ya Daesh na PKK
na kuuawa zaidi ya watu 180.
0 comments:
Post a Comment