Mbaroni Kwa Kuuza Mkono Wa Albino


Mtoto Mwigulu Matonange (10) Na Baba Yake
JESHI la Polisi mkoani Rukwa, likishirikiana na polisi mkoani Tabora pamoja na kikosi kazi maalumu cha kitaifa (TASK FORCE), limefanikiwa kuwatia nguvuni watu 9 waliokuwa wakisakwa kwa muda mrefu. Watu hao wamekuwa wakitafutwa kwa tuhuma za kumkata mkono mtoto Mwigulu Matonange (10), ambaye ni mlemavu wa ngozi na kuuuza kwa Sh milioni 600.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwarwanda, alisema watuhumiwa hao walikuwa wakisakwa kwa muda mrefu kutokana na mtandao mkubwa waliokuwa nao.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Weda Mashilimu (29), Nickon Kadogoo (25), Peter Msabato (32), Ignas Sungura (27), Faraja Mwezimpya (31) na Kurwa Hamisi (29) wote wakazi wa Kijiji cha Ilemba, mkoani Rukwa.

Kamanda huyo aliwataja watuhumiwa wengine ambao ni Hamis Mnywanywa, ambaye ni mganga wa jadi na mkazi wa Karema mkoani Katavi, James Paskali (24) mkazi wa Majimoto mkoani Katavi pamoja na Ibrahimu Tella (27), mkazi wa Kijiji cha Masanula-usule mkoani Shinyanga.

Kamanda alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni matokeo ya uchunguzi wa kina uliokuwa unafanywa na polisi hao kupitia mawasiliano ya simu na taarifa mbalimbali za kipelelezi.

Baada ya kuhojiwa, mtuhumiwa huyo alidai kuwa yeye na wenzake hao waliagizwa mkono huo na mganga wa jadi aitwaye Rashid Manywanywa, ambapo aliwaahidi angemlipa kila mmoja Sh milioni 600 iwapo wangempelekea mkono huo.

Alisema kuwa baada ya tukio la kumkata mtoto huyo mkono na kumpelekea mganga huyo, alidai kuwa hana fedha zote hizo, kwani wao walishindwa kutumia akili kwa kuwa hata yeye ni masikini angelipata wapi fedha zote hizo, hivyo hawezi kununua mkono huo.

“Baada ya kuona soko limeshindikana, ndipo walipoamua kufanya mawasiliano na watu wengine na kuhakikishiwa katika mikoa ya Tabora na Shinyanga kuna soko la uhakika, ndipo safari ya kuelekea huko ikaanza,” alisema kamanda huyo.

Kwa upande wake mganga huyo wa jadi, alikiri kuwaagiza watuhumiwa hao mkono huo na kudai kuwa alitaka kuutumia kutengenezea chombo cha usafiri ambacho alidai kuwa ni ungo ambao unatumika na wachawi kusafiria nyakati za usiku.

CHANZO:MTANZANIA
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment