VATICAN CITY
Katika hatua inayoonekana kuwa ya kihistoria, Rais wa
Palestina Mahmoud Abbas amefungua ubalozi wa nchi yake mjini Vatican.
"Leo tulikutana na Papa Francis. Ni matumaini yangu
kuwa mataifa mengine yatafuata mfano wa Vatican na kulitambua taifa na dola ya
Palestina," Abbas aliwaambia waandishi wa habari baada ya sherehe ya
ufunguzi wa umbalozi huo unaopatikana katika Mtaa wa Porta Angelica.
Vatican iliitambua Palestina kama taifa na dola mwaka 2005.
Kuhusu ahadi yenye utata ya Rais mteule wa Marekani Donald
Trump kuwa atauhamisha ubalozi wa Marekani kutoka mjini Tel Aviv kwenda eneo
linalokaliwa kimabavu la Jerusalem Mashariki, Abbas alisema kuwa hatua hiyo
itakuwa na madhara kwa mchakati wa amani.
"Tunasubiri kuona kama itatokea. Ikitokea,
haitasaidia suala la amani na ni matumaini yetu kuwa haitatokea," alisema.
Baada ya kauli yake hiyo, Abbas aliingia katika ubalozi
huo mpya na kupandisha bendera ya Palestina.
Askofu mkuu Angelo Becciu alihudhuria shughuli hiyo
akiiwakilisha Vatican.
Jumapili ya leo Ufaransa inatarajiwa kuandaaa mkutano wa
kimataifa mjini Paris unaolenga kufufua majadiliano kati ya pande mbili za
mgogoro wa Mashariki ya Kati.
Wakati utawala wa Israel ukidai kuwa Jerusalem Mashariki
ni “mji mkuu wake wa milele” baada ya kuukalia kwa mabavu wakati wa vita vya
mwaka 1967, jumuiya ya kimataifa haitambui madai hayo, na balozi za kigeni ziko
mjini Tel Aviv.
Baada ya uhusiano mbaya kati ya Rais wa Marekani
anayeondoka Barack Obama na Waziri Mkuu wa utawala wa Israel Benjamin
Netanyahu, kuna wasiwasi wa namna utawala wa Trump utakavyoathiri uhusiano kati
ya Marekani na Israel ambao ni washirika wa muda mrefu.
0 comments:
Post a Comment