Rais wa Gambia Yahya Jammeh |
Rais Yahya Jammeh wa Gambia ametangaza wazi kuwa hatong’atuka
madarakani licha ya kushindwa na kiongozi wa upinzani Adama Barrow kwenye
uchaguzi wa urais uliofanyika mapema mwezi huu.
Katika maelezo yake kwenye televisheni ya serikali,
pamoja na mambo mengine alilaani hatua ya usuluhishi inayofanywa na viongozi wa
Jumuiya ya Kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), ambao wamekuwa
wakijaribu kumshawishi akabidhi madaraka kwa amani wakati muda wake
utakapomalizika tarehe 18 Januari.
“Mimi sio mwoga. Haki yangu haiwezi kuzimwa na kukiukwa.
Huu ni wadhifa wangu. Hakuna anayeweza kuninyima ushindi isipokuwa Mwenyezi
Mungu,” alisema rais huyo ambaye amekuwa akidai kuwa uchaguzi ulikuwa na kasoro
nyingi.
Awali Jammeh aliyakubali matokeo ya uchaguzi huo
uliofanyika Desemba 1, ambapo Barrow alitangazwa kuwa mshindi, lakini alitengua
kauli yake wiki moja baadaye na kutaka uchaguzi urudiwe.
Hatua yake ya kuyakataa matokeo iliibua wasiwasi katika
taifa hilo na kusababisha jumuiya ya kimataifa kumshinikiza ayakubali matokeo
na kung’atuka madarakani. Wiki iliyopita ECOWAS ilisema kuwa Jammeh anapaswa
kuondoka madarakani mwezi ujao na kuahidi kuchukua hatua zote za lazima kuhakikisha
matokeo ya uchaguzi huo yanaheshimiwa.
Hata hivyo, katika kauli yake ya jana, Jammeh alisema
kuwa mikutano yake na wasuluhishi wa ECOWAS ilikuwa ya “utaratibu tu” na kwamba
hatong’atuka.
Uamuzi wake huu unatarajiwa kuibua mivutano zaidi katika
nchi hiyo ambapo jeshi limeshawekwa tayari huku likiwa limeyadhibiti makao
makuu ya tume ya uchaguzi katika hatua ambayo inaelezwa kuwa rais huyo
anajaribu kuonesha misuli yake.
Kiongozi wa upinzani nchini Gambia Adama Barrow (katikati) baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi Desemba 2, 2016 |
Naye msemaji wa upinzani, Halifa Sallah, jana alisema
kuwa Jammmeh hatoshitakiwa kwa kuyakataa matokeo kama atafanya uamuzi wa
kukabidhi madaraka kwa amani.
“Rais mteule Barrow anasema kuwa ataamiliana na rais Yahya
Jammeh kama kiongozi mstaafu wa nchi na atakuwa akichukua ushauri wake,” Sallah
alisema. Alisema kuwa Jammeh hana mamlaka ya kikatiba ya kubaki madarakani
baada ya mwezi Januari, huku akionya kuwa rais yeyote anayepoteza uhalali wa
kikatiba anakuwa muasi.
Marekani, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na
mashirika ya kimataifa yametoa wito wa makabidhiano ya madaraka kwa amani.
Rais Francois Hollande wa Ufaransa ambayo ilikuwa koloni
lake, amesema kuwa matokeo ya uchaguzi hayakuwa na shaka yoyote na kwamba
Barrow anatakiwa kuapishwa mapema iwezekanavyo.
Jammeh aliingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi
mwaka 1994 na amekuwa mamlakani tangu wakati huo.
0 comments:
Post a Comment