Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast |
ABIDJAN, Ivory Coast
Muungano unaotawala nchini Ivory Coast umeshinda
uchaguzi na kunyakua viti 167 vya ubunge kati ya viti 255.
Matokeo hayo yamethibitishwa na tume ya uchaguzi ya nchi
hiyo jana jioni.
Akizungumza na waandishi wa habari, mwenyekiti wa Tume
Huru ya Uchaguzi, Youssouf Bakayoko, amesema kuwa chama cha Watetezi wa Demkrasia
na Amani (RHDP) kilichukua nafasi ya kwanza kwa kupata asilimia 65.7 ya viti
kikifuatiwa na wagombea huru waliopata asilimia 29.
Muungano wa Demokrasia na Amani nchini Ivory Coast kimechukua
nafasi ya tatu kikiwa na viti sita (asilimia 2.36). Chama cha Rais wa zamani wa
nchi hiyo, Laurent Gbagbo cha FPI, kilipata viti vitatu.
"Tuna wabunge 254 waliochaguliwa, wanaojumuisha
wanaume 225 na wanawake 29," alisema Bakayoko.
Upigaji kura wa jimbo lililobaki utafanyika ndani ya
siku 15 katika wilaya ya Guiglo magharibi mwa nchi hiyo. Mchuano utakuwa kati
ya mgombea huru na yule wa RHDP.
Mwezi jana wapiga kura walipiga kura kwa wingi kupitisha
katiba mpya ambayo inampa fursa Rais Alassane Ouattara kugombea muhula wa tatu.
Ouattara aliyeingia madarakani mwaka 2010 alichaguliwa
tena kwa muhula wa pili mwezi Oktoba mwaka 2015.
Ivory Coast ilitumbukia katika ghasia za baada ya
uchaguzi wa mwaka 2010 ambazo zilisababisha vifo vya watu wasiopungua 3,000.
Rais wa wakati huo, Gbagbo alikataa kuyakubali matokeo
ya uchaguzi, na wafuasi wake walidai kuwa Ouattara hakuwa raia halisi wa nchi hiyo.
Gbagbo, ambaye alitawala kati ya mwaka 2000 na 2010, kwa
sasa anashikiliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu iliyo mjini Hague, akishitakiwa
kutenda uhalifu dhidi ya binadamu.
0 comments:
Post a Comment