Rais Joseph Kabila |
Serikali na upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo wamefikia muafaka wa makubaliano ambayo yatamrhusu Rais Joseph Kabila kubaki
madarakani kwa mwaka mmoja zaidi kwa sharti la kutogombea muhula wa tatu,
upinzani umesema.
“Kabila atabaki kwa mwaka mmoja zaidi,” kiongozi wa
upinzani Martin Fayulu amesema leo Ijumaa na kuongeza kuwa “hatoruhusiwa
kugombea muhula wa tatu.”
Mkataba huo kati ya pande mbili umekuja baada ya makumi
ya watu kuuawa katika maandamano dhidi ya serikali yaliyofanyika wiki hii. Umoja wa Mataifa umesema leo Ijumaa kuwa
kiasi cha watu 40 waliuawa.
Msemaji wa serikali alikataa kutoa maelezo kuhusu
kilichomo kwenye makubaliano hayo, ambayo yatahitaji kukubaliwa na wajumbe wote
wa mazungumzo yanayosimamiwa na viongozi wa Kanisa Katoliki nchini humo.
Jean Marc Kabund ambaye ni katibu mkuu wa chama kikuu
cha upinzani cha UDPS, alionya kuwa mkataba huo bado haujahitimishwa.
“Leo ni siku ya mwisho ya mazungumzo ,” alisema na
kuongeza, “yanayoweza kufaulu au kuvunjika.”
Muhula wa pili wa Rais Kabila ulimalizika siku ya
Jumanne. Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, rais mpya anatakiwa kuchaguliwa
sasa. Hata hivyo, bwana Kabila ameendelea kubaki madarakani baada ya uchaguzi
uliotakiwa kufanyika mwezi uliopita kuahirishwa kwa sababu ya kile ambacho
serikali ilisema ni kutokamilika kwa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura.
Picha iliyochukuliwa Desemba 20, 2016, ikiwaonesha watu wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya maandamano katika mtaa wa Yolo mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. |
Rais Kabila amekuwa akituhumiwa kufanya njama za kubaki
madarakani. Hata hivyo, wafuasi wake wanasema kuwa anatekeleza matakwa ya
kikatiba lakini kuondoka madarakani kunaweza kusababisha vita vya kugombea
madaraka na kuyaweka maisha yake hatarini.
Baba yake, mzee Laurent Kabila, ambaye alikuwa rais wa
nchi hiyo aliuawa mwaka 2001 na tangu wakati huo hakujawa na ubadilishanaji wa
madaraka kwa njia ya amani.
Alichukua madaraka siku kumi baada ya kuuawa kwa baba
yake.
Maandamano na mauaji ya wiki hii yameibua wasiwasi
kwamba taifa hilo linaelekea kwenye ghasia na vurugu kubwa.
0 comments:
Post a Comment