Ndege iliyotekwa ya Shirika la ndege la Libya, Afriqiyah,
aina ya Airbus A320 ambayo ilikuwa ikifanya safari za ndani imetua katika
Uwanja wa Ndege wa Malta.
Mapema leo Waziri Mkuu wa Malta, Joseph Muscat,
aliandika ujumbe katika akaunti yake rasmi ya Twitter kuwa ametaarifiwa kuwa
ndege hiyo imetekwa.
"Nimetaarifiwa juu ya utekaji nyara wa ndege ya
Libya inayofanya safari za ndani ambayo ilielekezwa Malta. Maafisa wa usalama
na shughuli za dharura wako katika hali ya utayari," aliandika Waziri Mkuu
huyo.
"Ndege ya Afriqiyah kutoka Sabha kwenda Tripoli ilielekezwa
na kutua Malta. Maafisa wa huduma za usalama wanafanya mawasiliano na watekaji,"
ulisomeka ujumbe huo.
Dauru kutoka ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa
nchini Libya zinasema kuwa mazungumzo yanaendelea ili kuhakikisha kuwa abiria
wote wanakuwa salama.
Watekaji wawili waliwatisha marubani kuwa wamebeba
mabomu, wakawalazimisha kutoka nchini Malta badala ya uwanja wa Mitiga mjini
Tripoli.
Utambulisho wa watekaji hao haujawekwa wazi. Inasemakana
wamekubali kuweka chini silaha zao.
Duru za serikali ya Malta zinasema kuwa ndege hiyo ilikuwa
imebeba watu 118, wakiwemo wafanyakazi saba wa ndege. Taarifa zinasema kuwa
abiria wameachiwa huru.
Tangu mwaka 2011, Libya imekuwa katikati ya ghasia
kufuatia mapinduzi yaliyomuondoa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar
Gaddafi, ambaye baadaye aliuawa. Aidha, Umoja wa Kujihami wa nchi za Magharibi,
NATO, ulijiingiza katika mgogoro huo.
0 comments:
Post a Comment