WATU 48 waliuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia
mji wa Mpeketoni, Kaunti ya Lamu usiku wa kuamkia leo katika pwani ya Kenya.
Shambulio hilo lilitekelezwa na washambulizi 50
waliokuwa wamejihami kwa silaha nzito kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na
serikali leo.
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema idadi ya
waliofariki ni 48, ingawa polisi walikuwa wamethibitisha vifo vya 26 pekee.
Katibu Mkuu wa shirika hilo Abbas Gullet alisema wawili
walijeruhiwa na wanatibiwa katika hospitali iliyo karibu.
“Tumekusanya miili 26 ambayo tumepeleka katika chumba
cha kuhifadhia maiti. Tunaendelea kusaka miili zaidi,” Bw Benso Maisoti ambaye
ni Kaimu Kamishna wa Wilaya aliliambia shirika la AFP.
Hata hivyo imeripotiwa leo asubuhi kuwa mji wa Mpeketoni
ambao mashambulizi yalifanyika uko katika hali ya utulivu.
Washambuliaji hao walitekeleza tendo hilo kutoka kwenye
magari mawili ya usafiri pamoja na kuchoma moto hoteli mbili, kwa mujibu wa ripoti
ya maafisa wa serikali. Kwa mujibu wa maafisa hao wengi wa waathiriwa walipigwa
risasi vichwani.
Mlinzi wa Kamishna wa Lamu Bw Leonard Omollo alikuwa
miongoni mwa watu waliouawa.
Maafisa wameongeza kusema kuwa miili 13 ilipatikana katika
makao ya Mama Ngina na mingine Saba kutoka kwa Hoteli ya Capital.
Miili mingine miwili ilipatikana katika Jumba la Wageni
la Breeze View huku miili zaidi ikiwa imetapakaa kote mjini.
Msemaji wa Polisi Zipporah Mboroki awali alikuwa amesema
walikuwa wamepata miili 14 ingawa idadi hiyo ilitarajiwa kuwa zaidi.
Washambuliaji hao vile vile walivunja benki tatu ambazo
ni Kenya Commercial Bank, Equity na Cooperative. Hata hivyo haijabainika ikiwa
waliiba pesa au la.
SERIKALI YA KENYA YAKOSOLEWA
Chama cha ODM kiliomboleza waliouawa Mpeketoni, Lamu na
kusema ni jukumu la Serikali ya Kitaifa kuhakikisha usalama wa raia popote
nchini humo.
Katibu Mkuu wa chama hicho Prof Anyang' Nyong'o kupitia
taarifa aliitaka Serikali ichukue hatua upesi kudhibiti hali Lamu na maeneo
mengine ya nchi yaliyo hatarini.
Baadhi ya watu walitoa wito kwa Rais Kenyatta kuwafuta
kazi wakuu wa usalama.
“Mheshimiwa Uhuru lazima afanyie mabadiliko baraza lake
la mawaziri na awastaafishe wakuu wake wa usalama upesi kwa maslahi ya
taifa,” alisema wakili mashuhuri
Ahmednasir Abdullahi kupitia Twitter.
0 comments:
Post a Comment