MMEA wa asili unaostawi kwa wingi ndani ya Hifadhi ya
Taifa ya Kitulo, maarufu kwa jina la Chikanda, upo hatarini kutoweka kutokana
na kuvunwa kiharamu na watu wanaoamini unasaidia kupunguza makali ya Ukimwi.
Zao litokanalo na mmea huo linafanana na kiazi mviringo
, linadaiwa kuwa na soko kubwa katika nchi za Zambia na Malawi. Tofauti na
viazi vya kawaida, katika shina lake Chikanda huzaa kiazi kimoja pekee.
Kaimu Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo iliyopo Matamba
wilayani Makete, mkoani Iringa, Pius Mzimbe, alisema uchunguzi waliofanya
katika nchi hizo unaonesha viazi hivyo vya Chikanda hutengeneza dawa kwa
matumizi ya binadamu na pia kwa ajili ya chakula.
Akizungumza na wanahabari waliotembelea hifadhi hiyo
hivi karibuni, alisema wavunaji haramu huingia kinyemela katika hifadhi hiyo
yenye milima mingi na kuvuna mimea hiyo na huuza kwa Sh 80,000 hadi Sh 100,000
kwa debe katika nchi hizo.
Kwa mujibu wa Mzimbe, kiazi cha mmea huo, kipo kwenye
kundi la nyara za Serikali na kwamba anayevuna au hata kupanda ndani na nje ya
hifadhi akibainika anahesabiwa amefanya kosa la jinai.
“Yapo madai
kwamba watu wanaohitaji aina hiyo ya kiazi kitokanacho na mmea huo wamekuwa
wakiwatumia wenyeji wa maeneo haya, kufanya uvunaji huo haramu na hivyo
kuathiri uoto wa asili wa hifadhi hii,” alisema.
Hata hivyo Mzimbe alikanusha kuwepo kwa utafiti wa
kisayansi unaothibitisha kwamba mmea huo una uwezo wa kweli wa kuwatibu watu
waliopungukiwa na kinga za mwili kutokana na Ukimwi.
Katika kukabiliana na majangili wanaovuna mmea huo,
alisema wanatumia kitengo chao cha ulinzi na intelejensia ambacho kwa kiasi
kikubwa kimeanza kufanikiwa kuwadhibiti.
Mhifadhi wa Utalii katika hifadhi hiyo, Rimus Mkongwe
alisema ndani ya hifadhi hiyo kuna aina 40 za mmea huo. Hata hivyo alisema
unaotakiwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu ni unatoa majani mawili.
Alisema taarifa walizonazo kutoka katika nchi
zinazonunua kiazi kitokanacho na mmea huo zinaonesha kwamba kinaliwa zaidi na
matajiri wakubwa wa nchi husika.
0 comments:
Post a Comment