Rais wa Colombia Juan Manuel Santos akisherehekea baada ya kushinda uchaguzi mji Bogota, Juni 15, 2014. |
Matokeo
rasmi yanaonesha kuwa Rais Juan Manuel Santos wa Colombia ametetea nafasi yake katika
marudio ya uchaguzi yaliyofanyika hivi karibuni na hivyo kuendelea kuiongoza
nchi hiyo kwa mhula wa pili.
Takwimu kutoka tume ya uchaguzi ya nchi hiyo zimeonesha kuwa bwana
Santos ameshinda kwa asilimia 50.95 ya kura, huku mpinzani wake wa mrengo wa
kihafidhina Oscar Ivan Zuluaga akifuatia kwa asilimia 45. Asilimia 4.03 ya kura
ziliharibika.
Ushindi wa bwana Santos unatazamwa kama kibali cha kuendelea na
mazungumzo ya amani na waasi wa (FARC). Santos aliwataka wananchi wa Colombia
kuchagua kati ya “mwisho wa vita au vita visivyokuwa na mwisho.”
Mpinzani wake bwana Zuluaga, ambaye kwa muda mrefu amekuwa
akipinga mazungumzo hayo ya amani, katika kampeni zake alitaka yawekwe masharti
magumu kama sharti la kufikia kwa muafaka wowote.
Santos anasema kuwa anatarajia muafaka wa mzozo huo utasainiwa
mwishoni mwa mwaka huu.
Serikali ya Colombia na waasi wa FARC wamekuwa wakifanya
mazungumzo ya amani katika mji mkuu wa Cuba, Havana, tangu Novemba 2012, katika
jitihada za kujaribu kukomesha mgogoro huo uliodumu kwa miongo mingi.
Kundi la FARC ndio kundi la muda mrefu zaidi katika eneo la Amerika
ya kusini na limekuwa likipigana na serikali tangu mwaka 1964. Kundi hilo
linaelezewa kuwa na wapiganaji wapatao 8,000 wanaofanya harakati zao katika
misitu ya mashariki mwa taifa hilo.
Serikali ya Colombia inakadiria kuwa watu 600,000 wameuawa na wengine
zaidi ya 4.5 wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita.
0 comments:
Post a Comment