Raia wa Libya leo wamemiminika kwenye vituo vya
kupigia kura kuwachagua wagunge katika uchaguzi unaotazamwa kama muhimu sana
kwa mustakbali wa taifa hilo ambalo limekumbwa na mizozo ya kisiasa na ghasia
za vita na mapigano.
Uchaguzi wa leo wa kuwania viti 200 vya bunge ni wa pili
tangu kuanguka kwa utawala wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar
Gaddafi mwaka 20011.
Aidha, uchaguzi huo unatazama kama hatua muhimu katika
safari ya Libya kuelekea kwenye utawala wa kidemokrasia na uthabiti wa kisiasa.
Wagombea wapatao 2,000 wanachuana kuingia katika bunge
jipya ambalo litaitwa Bunge la Wawakilishi.
Uchaguzi huo unafanyika bila chama chochote cha kisiasa.
Katika juhudi za kuondosha minyukano ya kisiasa ndani ya vyama, ambayo
ilidhoofisha uchukuliwaji wa hatua za maamuzi muhimu na kusababisha mzozo baina
ya mawaziri wakuu wawili mahasimu mwezi Mei, wagombea wanawania nafasi hizo
kama wagombe huru badala ya kuwakilisha vyama.
Nchi hiyo inahitaji serikali na bunge linalofanya kazi
ili kuwa na nguvu dhidi ya wanamgambo wenye silaha, ambao walisaidia kumuondoa
Kanali Gaddafi lakini kwa sasa wanakataa kuweka silaha chini na hawaitambui
mamlaka yoyote.
Aidha, Libya inakabiliwa na mgogoro wa kibajeti kutokana
na wimbi la maandamano kwenye viwanda vya mafuta na hatua ya wanamgambo kuyasshikilia
maeneo muhimu ya uzalishaji na hivyo kuzorotesha uzalishaji wa nishati hiyo
ambayo ni uti wa mgongo wa nchi hiyo.
Wakati huo huo, wananchi wa Libya wanahofia kwamba
uchaguzi huo unaweza kuzalisha bunge lingine la mpito. Tume maalumu iliyopewa
jukumu la kuandaa rasimu ya katiba mpya haijakamilisha kazi yake na hivyo
kuacha maswali mengi juu ya aina ya mfumo wa kisiasa utakaofuatwa na taifa
hilo.
Uchaguzi huo umeitishwa mwezi mmoja baada ya serikali
kudai kuwa jenerali mmoja wa jeshi wa zamani alikuwa akipanga kufanya
mapinduzi.
0 comments:
Post a Comment