MJUE BILIONEA ALIVYOPANGA MAUAJI YA MFANYA BIASHARA MWENZAKE HUKO KILIMANJARO

MFANYABIASHARA bilionea anayemiliki vitalu vya kuchimba madini ya tanzanite huko Mirerani mkoani Manyara, Joseph Damas, maarufu kwa jina la ‘Chusa’, ndiye anayedaiwa kupanga mauaji ya bilionea mwenzake wa madini, Erasto Msuya.
Msuya aliuawa kwa mtutu wa bunduki Agosti 7 mwaka jana saa 6 mchana barabara ya Moshi-Arusha eneo la Mjohoroni, Wilaya ya Hai, Kilimanjaro baada ya kumiminiwa risasi zaidi ya 20.
Kwa mujibu wa maelezo ya mashahidi 57 yaliyosomwa Juni 10, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi, Munga Sabuni, tajiri huyo anadaiwa kufanikisha mipango ya kumuua Msuya ikiwemo kutoa pesa zilizofanikisha wauaji kutekeleza uasi huo.
Akisoma maelezo hayo ambayo yatatumiwa na upande wa mashitaka kujenga msingi wa kesi hiyo, wakili wa serikali, Stella Majaliwa, aliieleza mahakama kuwa mfanyabiashara huyo alipanga mauaji akilipiza kisasi kwa Msuya.
Akinukuu maelezo ya mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Shariff Mohamed, wakili huyo akisaidiwa na mwenzake Florentina Sumari, alibainisha kwamba mfanyabiashara huyo alitoa maelekezo ya kuuawa kwa Msuya akiwa mjini Babati, Manyara.
Huko inadaiwa mfanyabiashara huyo alikuwa akipatiwa matibabu akiwa chini ya ulinzi wa askari magereza kutokana na kutuhumiwa katika mauaji ya mfanyabiashara mwingine wa madini, William Mushi anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi.
Katika maelezo ya kukiri kuhusika kwenye mauaji hayo, mshitakiwa huyo alidai kisa cha kutekeleza mauaji hayo ni madai kwamba Msuya alitoa fedha ili mfanyabiashara huyo asiachiliwe huru katika mauaji ya Mushi.
“Chusa aliniambia mateso yote ninayoyapata hapa ni kwa sababu ya Erasto maana ametoa pesa nyingi ili niunganishwe kwenye hii kesi, aliniomba nifanye kazi ya kumtoa roho Erasto na atagharamia kila kitu,” alidai Shariff katika maelezo yake ya maungamo.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, mshitakiwa huyo baada ya kutoka Babati alirudi siku nyingine na kukutana na mfanyabiashara huyo akishikiliwa na akamtaka kwa mara nyingine afanye hiyo kazi na kama atashindwa, mfanyabiashara huyo aliahidi kuifanya mwenyewe.
Mshitakiwa huyo aliendelea kueleza, mfanyabiashara huyo aliomba atafutwe mtu aitwaye Mredii ili amuue Erasto na alitekeleza jukumu hilo. Alikutana na Mredii ambaye katika kesi hiyo anatajwa kwa jina la Jumanne Mvungi akiwa mshitakiwa wa pili.
Wawili hao wanadaiwa kukutana ambapo Mredii alidai kazi hiyo itafanywa na watu wanne ambapo namba mpya sita za simu zilitengenezwa na kununua simu mpya nne zilizofanikisha mauaji hayo.
Naye Jumanne Mvungi ‘Mredii’ katika maelezo yake alidai Julai 26 mwaka jana alifuatwa na mshitakiwa wa kwanza na kumweleza kuwa kuna kazi ya kumuua Erasto na kwamba Chusa analalamika kuwa anamfuatilia kwenye biashara zake.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo anadai katika maelezo yake kuwa alimweleza Shariff hatoweza kuifanya kazi hiyo japo yupo tayari kumtafutia vijana wa kuifanya.
Akadai baada ya maelezo hayo alipewa sh 300,000 na mshitakiwa wa kwanza na kujaziwa mafuta kwenye gari lake kisha kusafiri hadi Babati alikokutana na mtu mwingine aitwaye Ally Msuya na kumweleza juu ya mpango wa kumuua Erasto.
Siku ya mauaji ilipofika mshitakiwa wa kwanza alikiri kuwa ndiye aliyebeba silaha aina ya SMG iliyotumika katika mauaji hayo hadi eneo la King’ori mkoani Arusha na kuikabidhi kwa Karim Kihundwa ambaye ni mshitakiwa wa tano.
Alidai baada ya kuikabidhi kwa Kihundwa, alirejea Arusha huku akisihi wasichukue kitu chochote kutoka kwa marehemu pindi watakapotekeleza mauaji hayo ikiwa ni maelekezo kutoka kwa Chusa.
Kwa mujibu wa maelezo ya mshitakiwa huyo, baada ya mauaji hayo mshitakiwa wa pili na wa sita, Sadik Jabir ‘Msudani’ walimfuata hadi Arusha na aliwapa sh milioni 10 huku sh milioni sita nyingine akiahidi kuwalipa baada ya kukutana na Chusa.
Mshitakiwa huyo akahitimisha maelezo yake kuwa baada ya mauaji hayo alimfuata Chusa mjini Babati hospitali alipokuwa anashikiliwa na askari magereza na baada ya kumweleza kuwa kazi imefanyika, alifurahi sana.
Pamoja na maelezo hayo, Aprili 16 mwaka huu Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Elieza Feleshi, alimfutia mashitaka ya mauaji mfanyabiashara huyo chini ya kifungu cha 91 cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai.  CHANZO  CHA  HABARI  '-TANZANIA  DAIMA
Share on Google Plus

About www.habarika24.blogspots.com

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment