MWANAMUME ALIYEMUUMIZA MKEWE KWA SABABU YA CHAKULA AFUNGWA JELA

 

MWANAMUME mmoja huko Kenya aliyepatikana na hatia ya kumpiga mkewe na kumuumiza kwa madai kuwa alichelewa kumpa chakula cha mchana, amehukumiwa kwenda jela miezi mitatu ama alipe faini ya Sh5, 000 za Kenya.

Mahakama ya Eldoret nchini humo ilimpata Gideon Kenneth Gavana na hatia ya kumpiga mkewe na kumwacha na majeraha mabaya ya kichwa, miguu na mikono.

Hakimu Msimamizi mkuu Bw Samwel Mokua alitoa uamuzi huo baada ya Bi Sophia Gavana na wanawe wawili kutoa ushahidi mahakamani kuhusiana na kilichotokea siku hiyo.

Mahakama ilielezwa kuwa, mshtakiwa aliwasili nyumbani kwake katika eneo la Road Block mojawapo ya viungani mwa mji wa Eldoret mnamo Mei 24 mwendo wa saa saba mchana na kumkuta mkewe jikoni akiwa anaanda chakula cha mchana.

Bw Gavana alisemekana kuitisha chakula kwa njia isiyo ya kawaida na hata baada ya kuambiwa na mkewe kuwa asubiri, alikataa kata kata na kuongea kwa sauti ya juu kana kwamba alikuwa amenyimwa chakula hicho.

“Nilipomletea mume wangu chakula, alikuwa amekasirika na akataka nibadilishe sahani na nimwekee chakula kwenye sahani nyingine ambayo alisema aliipenda sana.

Nilipokuwa narudi ndani ya nyumba kuitafuta ile sahani, mume wangu alinishika kwa nyuma na kuniangusha chini kabla ya kuanza kunipiga kwa ngumi na mateke na hadi wanangu wawili walipoingilia kati na kuniokoa,” Sophia alisema.


Barua kutoka kwa daktari wa hospitali ya eneo hilo la Baharini Bonface Watila Ndula ilionyesha kuwa, ni kweli mlalamikaji alifikishwa katika kituo hicho cha afya akiwa na maumivu mabaya ya kichwa na sehemu nyingine za mwili.

CHANZO: Swahilihub.com
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment