Watu wasiojulikana wamemuua kwa kumpiga risasi
Mwenyekiti wa Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu nchini Kenya, Sheikh Mohammed
Idris, asubuhi ya leo katika eneo la Likoni, Mombasa.
Aidha, Sheikh Mohammed alikuwa mwenyekiti wa Masjid
Sakina mjini Mombasa ambao hivi karibuni ulidaiwa kuingia katika mzozo na
baadhi ya vijana ambao alikuwa akiwaona kuwa wenye msimamo mkali.
Polisi wanasema mwili wa marehemu ulipelekwa kwenye
chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Pandya.
Aidha, Polisi wanasema kuwa muuaji bado hajajulikana na
kwamba Sheikh aliuawa karibu na nyumbani kwake wakati akitoka msikitini. Kwa muda
sasa Sheikh Mohammed Idris alikuwa akielezea hofu yake ya kuuawa baada ya
kupewa vitisho mara kadhaa kutoka kwa vijana hao.
Mkuu wa upelelezi mjini Mombasa Henry Ondieki anasema
kuwa wanashuku kwamba Sheikh Idris ameuawa na mtu anayemjua vizuri na kwamba
walimfuatilia kwa muda mrefu kabla ya kumshambulia.
Taarifa za ndani zinadai kuwa Sheikh Idris alikuwa
mkosoaji mkubwa wa baadhi ya makundi ya vijana aliyoyatazama kama makundi yenye
msimamo mkali na kuwataka polisi kuwashughulikia wale aliodhani wanahusika na
kuwatia kasumba vijana hao kwa madai kuwa walikuwa wakisababisha ghasia kwa
jina la Uislamu. Msimamo wake huo uliwakasirisha vijana wengi waliomuona kama
msaliti.
Katika miezi ya hivi karibuni, mji wa Mombasa ambao ni
mji wa pili kwa ukubwa na kitovu cha utalii nchini Kenya, ni miongoni mwa miji
kadhaa ambayo imekuwa ikikumbwa na ghasia mbalimbali huku viongozi kadhaa wa
kidini wakiuawa.
0 comments:
Post a Comment