Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
imetoa mapendekezo mapya ya kukabiliana na rushwa ikishauri sheria zirekebishwe
kuwabana wenye mali zilizopatikana kinyume cha sheria kushtakiwa na kufilisiwa.
Takukuru imependekeza kuifanyia marekebisho Sheria ya
Kupambana na Kuzuia Rushwa, ili kosa la rushwa liwe la uhujumu uchumi na
mhusika mwenye mali nyingi anaposhindwa kuthibitisha alivyozipata afikishwe
mahakamani na mali zake zitaifishwe.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea, alisema
hayo wakati wa majadiliano kwenye semina ya wabunge wa Chama cha Kupambana na
Rushwa (APNAC) iliyofanyika mjini hapa mwishoni mwa wiki.
Alisema sheria ya sasa ina upungufu mkubwa, hivyo
wanaona ni vema kama ingefanyiwa marekebisho ili kuipa nguvu ya kuwabana watoa
na wapokea rushwa pamoja na hao wenye utajiri mkubwa.
Alitaja kwa mfano, sheria ya sasa inatoa adhabu ya
kifungo au kulipa faini ya hela kwa mshitakiwa aliyetiwa hatiani na mahakama na
inatoa hiari kwa mahakimu kutoa moja ya adhabu kati ya hizo, hivyo wengi
wakipewa adhabu ya kulipa faini hawatashindwa.
“Hata kama atatozwa faini ya Sh. milioni 10,
watachangishana na mla rushwa ataachiwa huru huku akiendelea kumiliki mali
alizojipatia kwa rushwa,” alionya Dk. Hosea na kuongeza: “Tunapendekeza adhabu
iwe kifungo na kesi za rushwa ziwe katika kundi la kesi za uhujumu uchumi
baadhi ya nchi kama Nepal, Uingereza na Ethiopia wanafanya hivyo.”
Pia alisema wanataka sheria ya madaraka ya Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP) yapelekwa pia kwa Takukuru ili kukamata, kupeleleza, kuendesha
mashtaka na pia rushwa iwe na mahakama yake.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kufanya kazi hizo
haimaanishi kwamba Takukuru itakuwa inapokonya madaraka ya DPP.
Kuhusu watu wenye mali nyingi, alisema sheria iwatake
watu hao kujieleza namna walivyopata mali zao na kama wakishindwa basi
wafikishwe mahakamani na mali zao kutaifishwa.
“Hiyo itasaidia sana kupunguza rushwa,” alisema.Mapema
akifungua semina hiyo, Jaji Mkuu Mohammed Othman Chande, alisema katika
kutathmini mapambano dhidi ya rushwa, siku zote, habari mbaya za rushwa
zinachafua matendo au jitihada nzuri za kupambana na rushwa.
Akizungumzia rushwa wakati wa uchaguzi, alisema katika
uchaguzi mkuu uliopita, kulikuwa na mashauri 44 ya kupinga matokeo ya uchaguzi
huo na mengine yalihusisha vitendo vya rushwa katika kampeni za uchaguzi kwa
wagombea.
Alisema kwa mfano, baadhi ya makosa ni wagombea kutoa
chakula kwa wapiga kura, kuwapa fedha, kuwakodia magari ya usafiri kutoka
sehemu moja hadi vituo vya kupiga kura, kutoa ahadi ya kuboresha miundombinu
iwapo mgombea fulani atachaguliwa.
Aliwaambia wabunge hao kuwa kiwango cha kuthibitisha
makosa hayo ni cha jinai na siyo cha madai hivyo katika baadhi ya mashauri
kulikuwa hakuna ushahidi wa kutosha.
Pia alisema baadhi ya mashahidi walichelewa sana kutoa
taarifa tangu kutokea kwa tukio la rushwa na kwamba baadhi yao walijihusisha
katika rushwa. Akizungumzia rushwa mahakamani, alisema hakimu anayepokea rushwa
anafanya biashara haramu ya kumnyima mlalamikaji haki yake.
Alisema kwa mfano, hakimu anayeendesha kesi hawezi au
hatakiwi kukutana na mteja wa upande mmoja wa kesi nje ya mahakama kama vile
baa.
Kadhalika, alizungumzia pia kuhusu bajeti ndogo ambayo
Idara ya Mahakama inapata na akasema kwa mfano, sera ya serikali inataka
mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo wasikae kituo kimoja zaidi ya miaka mitatu,
lakini kiuhalisia wapo wanaokaa hata miaka 10 kituo kimoja.
Alisema hiyo inatokana na bajeti ndogo ambayo serikali
inaipatia mahakama na akafafanua kwamba ili mahakimu hao waweze kuhamishwa kwa
mujibu wa muda uliowekwa, gharama ya uhamisho zinakula fedha zote ambazo
wametengewa na serikali kwa mwaka.
Alitoa changamoto kwa wabunge kuongeza bajeti na kuwa na
Mfuko wa Mahakama kama ambavyo upo Mfuko wa Bunge.
Ofisa Habari wa Bunge, Owen Mwandumbya, akiwasilisha
mada kuhusu ‘Uhusiano kati ya Vyombo vya habari na Wanasiasa, alisema uhusiano
kati yao ni muhimu, lakini hautakiwa kuzidi sana.
Alisema uhusiano ukizidi sana unaweza kuathiri
upatikanaji wa habari kwa jamii, kwa kupewa habari ambazo wanasiasa wanazitaka.
Alisema habari za rushwa ni moja kati nyingi ambazo
zinapendwa kuandikwa au kutangazwa kwenye vyombo vya habari, hivyo zinaweza
kuwachafua wanasiasa kwa haraka zaidi.
“Kazi kubwa ya vyombo vya habari pamoja na suala la
kuelimisha lakini wanataka kufichua maovu na wanapofanya hivyo wanatarajia
hatua zitachukuliwa haraka dhidi ya wahusika,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment