Wadi us-Salaam, ambayo ina maana ya “Bonde la Amani”, ni
eneo la makaburi linalopatikana katika mji wa Najaf, nchini Iraq. Eneo hili
linajumuisha ukubwa wa ekari 1485.5 na mamilioni ya miili imezikwa hapo na
hivyo kulifanya kuwa eneo kubwa zaidi la makaburi duniani.
Mji wa Najaf ni miongoni mwa miji mkubwa zaidi nchini
Iraq. Eneo hilo lenye mabaki ya mamilioni ya miili ya wafu linatambaa umbali wa
kilometa 10. Aidha, Wadi Al-Salam ni eneo pekee la makaburi duniani ambapo bado
linaendelea kutumika tangu zaidi ya miaka 1,400 mpaka sasa.
Aidha, eneo hilo linaelezwa kuwa na makaburi ya watu
mashuhuri duniani, manibii na mitume, wafalme na masultan.
Miongoni mwa makaburi yanayopatikana hapa yamejengwa kwa
matofali na kuwa na ukubwa tofauti tofauti. Kuna makaburi yenye ukubwa wa
vyumba vya kulala ambayo yamejengwa na watu wenye uwezo wa kifedha na kuwekewa
minara na kuba juu yake. Pia kuna makaburi ya chini kwa chini ambapo ngazi za
kupanda na kushuka huko zimewekwa. Makaburi ya miaka ya 1930 na 1940 yana
muundo wa aina yake, yana urefu mpaka wa futi 10 na hivyo kuonekana kwa urahisi
zaidi.
Wakati wa vita vya Iraq mwaka 2003, wanamgambo
walilitumia eneo hilo kama maficho na kuweka mitego dhidi ya vikosi vya adui. Wamarekani
walikuwa hawezi kwenda huko, hivyo wanamgambo walikuwa wanapofanya mashambulizi
walikuwa wakikimbilia huko.
Ghasia ambazo zimeikumba Iraq tangu mwaka 2003 zimesababisha
eneo hilo kupanuliwa kwa asilimia 40 na kufikia takriban maili tatu za mraba. Eneo
hilo limekuwa likipanuliwa kila mwaka. Kwanza wakati wa uvamizi wa Marekani,
kisha ghasia za 2006-2007 ambapo Mashia na Masunni walikuwa wakiuana kwa
kiwango kikubwa, na hatimaye mwaka 2008 kati ya jeshi la Iraq na waasi. Hata katika
miaka ya hivi karibuni limekuwa likiongezeka ingawa kwa kiwango kidogo.
0 comments:
Post a Comment