MCHANGO WA MAANDISHI WA NDG. KABWE ZUBERI ZITTO, MB
KUHUSU BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
Mheshimiwa Spika, Kwanza kabisa napenda kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu za kuweza kuandika mchango wangu huu mdogo
kwenye mjadala wa Bajeti ya Serikali mwaka 2014/15. Kama wengi mnavyofahamu
mnamo tarehe 1 Juni mwaka 2014 nilimpoteza mama yangu mzazi na kumsitiri siku
iliyofuata tarehe 2 Juni, 2014. Huu ni msiba mkubwa sana kwangu na ndugu zangu
wote kwani mama yetu Bi. Shida Salum alikuwa nguzo katika familia. Nafahamu
kuwa jamaa na marafiki wa mama pia wamepoteza mtu wao muhimu sana. Napenda
kuwashukuru nyote kabisa kwa salamu zenu za pole kwetu. Sina namna ya kuelezea
shukrani zangu kwenu kwani Bi Shida kwangu alikuwa zaidi ya mama mzazi, alikuwa
rafiki, dada na nguzo. Ninamshukuru Allah kwa kuniwezesha kumwuguza na
kumsitiri mama yangu. Hakuna amali kubwa ambayo Mungu amenipa zaidi ya hiyo.
Nawashukuru tena nyote kabisa wabunge wenzangu kwa kushirikiana nami kwa namna
zozote zile kumwuguza na kumsitiri mama yangu. Mungu atawalipa malipo
yanayowastahili kwa amali na vitendo vyenu. Sisi kama familia tutaendelea
kumwombea dua mama yetu na kumtolea sadaka ili ahifadhiwe mahala pema.
Mheshimiwa Spika, ningependa niwe nanyi katika mjadala
huu muhimu wa kila mwaka wa Taifa letu. Hata hivyo bado Mungu hajaniwezesha
nguvu za kusimama na kuzungumza. Pindi nitakapowezeshwa nguvu hizo nitakuwa
nanyi kwa kipindi hicho nitakachojaaliwa ili kushiriki katika kazi za
kuendeleza Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumpongeza Waziri
wa Fedha ndugu Saada Salum kwa kuwasilisha Bajeti yake ya kwanza kabisa kama
Waziri wa Fedha wa pili Mwanamke wa nchi yetu. Nampongeza kwa kuchukua hatua
kadhaa za kuboresha usimamizi wa fedha za umma na hasa matamko aliyotangaza ya
kupambana na misamaha ya kodi ambayo imeongezeka mpaka kufikia asiliamia 3.5 ya
Pato la Taifa na asilimia 10 ya Bajeti ya Serikali. Misamaha ya Kodi mwaka
2012/13 ilifikia tshs 1.5 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 15 ya makusanyo
yote ya ndani na ni sawa na takribani fedha zote za kodi ambazo Serikali
ilikusanya kama kodi ya mishahara ya Wafanyakazi (PAYE). Hata hivyo, matamko ya
Serikali yana mapungufu makubwa sana na ni matamko yale yale yanayorudiwa kila
mwaka bila utekelezaji. Kuweka wazi misamaha ya kodi na watu au asasi
zilizofaidika na misamaha hiyo ni hatua nzuri lakini haitoshi kama hatua hiyo
haitaendana na kufanya ukaguzi wa misamaha hiyo. Kamati ya Bunge ya PAC ilitoa agizo
mwaka 2013 la kutaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kukagua
misamaha ya kodi kama matumizi mengine yeyote ya Serikali. Ieleweke kwamba
misamaha ya kodi ni ruzuku (subsidy), ni fedha ya Serikali ambayo iwapo
ingekusanywa ingekaguliwa kwa mujibu wa sheria. Matamko ya Serikali ya kuweka
wazi misamaha lazima yaendane na kuifanyia ukaguzi (auditing) na kuweka wazi
matokeo ya ukaguzi huo. Vilevile ni lazima sasa katika Sheria ya Fedha ya mwaka
2014/15 kuweka kipengele cha kuzuia misamaha ya kodi kuzidi asilimia moja ya
Pato la Taifa na kurekebisha Sheria ya Ukaguzi ya umma wa mwaka 2008 ili kumpa
mamlaka ya kisheria CAG kukagua misamaha ya kodi na kuweka wazi matokeo ya
ukaguzi huo kwa umma.
KODI KWA WAFANYAKAZI
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha ametangaza nafuu ya
kodi kwa wafanyakazi wa kima cha chini kutoka kiwango cha 13% mpaka 12%.
Kiwango hiki ni kidogo mno na hakimsaidia mfanyakazi kubakia na fedha kwa ajili
ya matumizi yake na pia kwa ajili ya kujiwekea akiba. Ni dhahiri kuwa PAYE ni chanzo
kikubwa sana cha mapato ya ndani ya Serikali. Kwa mfano mwaka 2013/14 Serikali
ilitarajiwa kukusanya tshs 1.5 trilioni kama PAYE ambapo tshs 1 trilioni kutoka
idara ya walipa kodi wakubwa na tshs 500 bilioni kutoka idara ya kodi za ndani.
Hata hivyo, utaona kuwa mapato haya ni sawa sawa na kodi inayosamehewa kupitia
misamaha ya kodi hivyo iwapo misamaha ya kodi ikipunguzwa mpaka kiasi cha
asilimia 1 ya Pato la Taifa, Serikali itakusanya kodi ya kutosha kuzipa pengo
la punguzo la kodi kwa wafanya kazi. Vile vile Serikali inapoteza kodi nyingi
sana kupitia ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni makubwa ya kimataifa
yanayowekeza hapa nchini (tax evasion and tax avoidance) kwa kiwango cha
asilimia 5 ya Pato la Taifa. Iwapo Serikali itajiunga na mikataba ya kimataifa
ya kupambana na ukwepaji kodi na pia kuimarisha kitengo cha kodi za Kimataifa
ili kupambana na Multinational Corporations ambao wanatumia njia mbalimbali
kuhamisha faida zao nje, kutangaza hasara hapa nchini na kukwepa kodi za
thamani ya zaidi ya shilingi trilioni mbili kila mwaka kwa mujibu wa takwimu za
Global Financial Integrity. Napendekeza kuwa kiwango cha chini cha kipato
(mshahara) kukatwa kodi kiwe shilingi 330,000 na kiwango cha chini cha kodi
kiwe asilimia 9 tu.
Mheshimiwa Spika, Kiwango hiki cha kodi pia kinawezekana
kwa Serikali kuchukua hatua dhidi ya matumizi mabovu ya Serikali. Kwa mfano,
kwa mujibu wa Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Serikali mwaka 2013, mfumo wa
kukagua utumishi wa umma umegundua kuwa jumla ya wafanya kazi wa Serikali 6500
walikuwa wameajiriwa mara mbili kwa majina yale yale, 2700 mara tatu na
kulikuwa na watumishi 2500 waliokuwa wanachukua mishahara miwli mpaka mitatu
kila mwezi. Baada ya mfumo wa Lawson kuanzishwa jumla ya wafanyakazi hewa
14,000 waligundulika katika jumla ya wafanyakazi 478,000 wa Serikali. Hatua ya
kuondoa matumizi mabovu kutokana na kulipa mishahara hewa pia inaweza kusaidia
kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi nchini. Serikali hutumia wastani wa
shilingi bilioni 360 kila mwezi kulipa mishahara ambapo katika hizo shilingi
bilioni Kumi kila mwezi zimekuwa zikilipwa kwa watumishi hewa. Nafuu ya kodi
kwa wafanyakazi nchini katika sekta zote na hasa wafanyakazi wa kima cha chini
kitachochea matumizi binafsi ya bidhaa na huduma na hivyo kuchangamsha uchumi
na kuwezesha uwekaji wa akiba nchini. Nashauri ukaguzi zaidi ufanyike katika
utumishi wa umma ili kumaliza kabisa tatizo la wafanyakazi hewa nchini.
Mheshimiwa Spika ninapongeza kuanzishwa kwa kodi ya zuio
kwa ada kwa Wakurugenzi wa makampuni na Mashirika. Kodi hii itaongeza mapato ya
Serikali. Hata hivyo kodi kama hii pia itozwe kwenye posho ambazo viongozi wa
kisiasa na watumishi wa Serikali wanalipwa isipokuwa posho ya kujikimu (per
diem). Vile vile uamuzi wa kuagiza Wizara, Idara na Wakala za Serikali
kukusanya maduhuli kwa kutumia mashine za kielektroniki ni uamuzi muhimu sana
ambao utaongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi. Kamati ya
PAC iliagiza jambo hili tangu mwaka 2013 na ninaamini kuwa Polisi wa Usalama
barabarani wataanza kutoa ‘traffic notifications’ kwa njia hii; pia Wizara ya
Ardhi wataanza kutoa Hati za Ardhi za kielektroniki na kukusanya maduhuli kwa
njia hii ikiwemo Wizara ya Nishati na Madini kwa tozo mbalimbali wanazotoza.
Juhudi zote hizi lazima zionekane kwa kupunguza mzigo wa kodi kwa Wafanyakazi
ambao kiukweli ni wachache (takribani 1.3 milioni) lakini wanabebeshwa mzigo
mkubwa wa kodi kuliko wawekezaji wakubwa.
Mheshimiwa Spika, Tanzania haiwezi kuendelea kuwa nchi
ambayo Serikali yake inaendeshwa na fedha za wafanyakazi, wafanyabiashara
wadogo na wahisani. Ni lazima makampuni makubwa ya uwezekaji nchini yashiriki
kuendesha Serikali kwa kulipa kodi stahili na kuondoa kabisa misamaha ambayo
haina mahusiano yeyote na ukuaji wa ajira nchini na kuongeza thamani ya mazao
yetu ya kilimo. Vile vile ni muhimu sana kuongeza juhudi za kukuza ajira ili
kuwa na wafanyakazi wengi ambao watapelekea kuongeza mapato ya Serikali badala
ya kukamua kundi dogo lililopo hivi sasa. Nchini Kenya kiwango cha chini cha
Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi (PAYE) ni asilimia 10 tu kwa sababu idadi ya
walipaji wa kodi hii wanafikia takribani milioni kumi wakati Tanzania ina
wafanyakazi wanaolipwa mishahara ya kila mwezi milioni 1.3 tu.
HIFADHI YA JAMII KWA WAKULIMA
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa
inaonesha kuwa Tanzania ina jumla wa mifuko mitano ya Hifadhi ya Jamii yenye
wanachama 1.3 milioni pekee. Idadi hii ya wanachama ni 6% ya nguvu kazi ya
Tanzania. Hata hivyo nguvu kazi ya nchi haipo kwenye wafanyakazi wa mishahara
pekee kwani asilimia takribani 70 ya Watanzania wanaishi vijijini na
kujihusisha na sekta ya Kilimo. Kwa kuwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii haijafikia
wakulima maana yake Watanzania wengi sana wanaishi ya mashaka kwa sababu hawana
Bima ya Afya, hawana mafao mengine ya muda mfupi na wala hawana pensheni. Hali
hii ni lazima kuirekebisha kama tunataka Taifa lenye maendeleo. Hifadhi ya
Jamii sio suala la pensheni tu bali pia ni suala la uwekezaji wa akiba
(savings) na uwekezaji wa ndani (investments).
Mheshimiwa Spika, Kasi ya ukuaji uchumi na uwekezaji
(Growth and investment rates) vina mahusiano chanya.Takwimu za Penn World
Tables (2002) zinaonyesha kuwa kwa nchi 38 za Afrika Kusini mwa jangwa la
Sahara wastani wa ukuaji uchumi ulikuwa 0.6% na wastani wa uwiano wa uwekezaji
na ukuaji uchumi ulikuwa 10%. Kwa nchi 9 za Asia (9 Asian 'miracle' economies),
wastani wa ukuaji uchumi ulikuwa 4.9% na wastani wa uwiano kati ya ukuaji
uchumi na uwekezaji ulikuwa 25%. Kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa lolote
duniani unahusiana moja kwa moja na utayari wa wananchi wa nchi hizo kuweka
akiba na kuwekeza vitega uchumi. Takwimu hizi zinaonyesha dhahiri kwamba ili
Afrika ipige hatua ni muhimu sana kuimarisha uwekezaji wa ndani ambao unatokana
na kiwango cha uwekaji akiba.
Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi wa kasi na haraka
hauwezekani bila ya sekta ya fedha iliyokita mizizi. Hata hivyo, kwa mujibu wa
Taarifa ya Hali ya Umasikini nchini (PHDR 2009) mfumo wa kibenki nchini kwetu
hautoi msaada wa kutosha kwa wafanyabiashara ndogondogo na wakulima. Mikopo kwa
uwekezaji wa ndani ni midogo sana kiasi kwamba haisaidii kuongeza uzalishaji
(productivity) na kuhimiza mabadiliko makubwa ya Uchumi (transformation of the
economy). Mikopo mingi inayotolewa na mabenki ni kwa matumizi binafsi ya watu
na mikopo mikubwa ni kwa shughuli za uchuuzi (trading) badala ya uzalishaji.
Hii inathibitishwa na Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2013 ambayo
inaonyesha kuwa katika mikopo ya thamani ya tshs 10.3 trilioni, ni asilimia 9
tu iliyokwenda sekta ya kilimo. 11.4% viwanda na 25% ilikwenda kwa wachuuzi.
Asilimia 17 ya mikopo ilikwenda kwa watu binafsi kwa ajili ya matumizi binafsi!
Kuna haja kubwa ya kufanya mabadiliko makubwa sana ya
kimuundo na kisheria na kisera ili kuhakikisha kuwa uzalishaji kwenye kilimo na
uongezaji thamani wa bidhaa za kilimo unapata uhakika wa fedha za mikopo. Benki
sio rafiki ya Masikini. Benki sio rafiki ya mkulima mdogo hapa nchini. Lazima
kubadilika kifikra na kuachana na mazoea. Ni lazima sasa kuweka vivutio kwa wakulima
kuweka akiba ya muda mrefu na kuondoa mwiko wa mkulima kutokuwa na pensheni.
Hifadhi ya Jamii kwa Mkulima ni suluhisho la kuongeza akiba nchini, kupanua
fursa za uwekezaji wa ndani tena kwenye kuongeza uzalishaji wa Kilimo na
kujenga jamii ambayo inahifadhiwa. Hifadhi ya Jamii kwa Mkulima pia itaongeza
ushindani dhidi ya mabenki katika soko la mikopo midogo midogo na hivyo
kumfaidisha mkulima.
Mheshimiwa Spika, mabilioni ya fedha tunayoona
yanamilikiwa na mabenki, mifuko ya hifadhi ya jamii, kampuni za bima na asasi
za uwekezaji ni matokeo ya kukusanya viakiba vya mtu mmoja mmoja kutoka kwa
mamilioni ya watu. Kazi ya asasi za fedha ni kukusanya mabilioni haya na
kuyaelekeza kwenye uwekezaji wa miradi mikubwa ianyofanywa na wafanyabiashara
na hata miradi midogo kwa wafanyabiashara wadogo. Katika bara la Afrika, hivi
sasa watu masikini wanaweka akiba zao katika vyama vya kuweka na kukopa
(SACCOS). Hii ni hali halisi Tanzania, hali ambayo lazima tuijenge kwani
mabenki hayapendi kuendesha akiba ndogondogo za watu masikini. Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii imeanza mafao ya mikopo kwa SACCOS za wanachama wao na hivyo
kuweza kukopa kwa lengo la kuendesha maisha yao kwa kuongeza uzalishaji hasa
kwenye Kilimo. Wafanyakazi wa Sekta rasmi wametungiwa sheria kwamba ni lazima
sehemu ya mishahara yao wakatwe kama akiba ya uzeeni na majanga mengine.
Waajiri wao pia hukatwa fedha kuchangia pensheni za wafanyakazi wao. Mkulima
hana sheria ya kumlazimisha kuweka akiba (na sio lazima kuwepo kwa sheria hiyo)
na pia hana ‘mjomba’ wa kumchangia sehemu ya pensheni yake. Hata hivyo Mkulima
anachangia 25% ya Uchumi wa Tanzania (GDP) na pia fedha za kigeni. Mchango wa
bidhaa za kilimo kwenye mauzo nje umekuwa mdogo kwa sababu wakulima wananyonywa
na mabenki na hawana fursa ya mikopo ya kupanua mashamba yao, kununua pembejeo
na kufikia masoko mazuri ya bidhaa zao.
Mheshimiwa Spika, Hali ya Uchumi wa Taifa 2013 inaonesha
kuwa 20% ya mapato ya fedha za kigeni nchini yanatoka kwenye bidhaa za kilimo
ambacho ni Pamba, Kahawa, Tumbaku, Chai, Korosho, Karafuu na Katani. Mazao haya
yanaingiza jumla ya dola za kimarekani 867 milioni. Uchumi wetu hauwezi kuondoa
umasikini kwa sababu shughuli zake zimejikita kwenye sekta ya madini ambayo
inachangia ajira kiduchu (an enclave) lakini inachangia 40% ya mauzo nje.
Uchumi wetu ni egemezi na tegemezi kwa sekta moja tu jambo ambalo ni hatari
sana kwa ustawi wa maisha ya wananchi. Ni wajibu wa Serikali kuweka mazingira
ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya Kilimo na hivyo kuongeza mapato ya fedha za
kigeni na kuondoa umasikini vijijini. Mauzo ya bidhaa za kilimo nje yameshuka
kwa kiwango cha asilimia 9, zao la Tumbaku ambalo ndio linaongoza kwa kuingiza
fedha za kigeni dola za marekani 307 milioni (zaidi ya shilingi bilioni 500 za
kitanzania), mauzo yake yaliporomoka kwa kiwango cha asilimia 12 kutokana na
wakulima kutotumia mbolea kwa sababu ya kukosa mikopo katika mabenki
kulikosababishwa na unyonyaji wa zaidi ya shilingi bilioni 28 kwa mujibu wa
taarifa ya ukaguzi. Mauzo ya Pamba yalishuka kwa asilimia 32 kutokana na
mgogoro wa bei uliosababishwa na kutokuwepo kwa sera ya kufidia bei kwa
wakulima (price stabilisation).
Mheshimiwa Spika, suluhisho la mambo yote haya ni
kuingiza wakulima kwenye hifadhi ya jamii ili waweke akiba, wapate mafao ya
muda mfupi na mrefu na wapate mikopo kupitia vyama vyao vya ushirika vya kuweka
na kukopa(AMCOS). Mabenki hayataendelea tena kunyonya wakulima kwa sababu riba
zinazotolewa kwa mikopo ya SACCOS/AMCOS ni nafuu na zinaendana na hali halisi
ya wakulima. Kupitia kujiunga kwao katika Hifadhi ya Jamii, Fao la fidia ya bei
laweza kuanzishwa ili kuwafidia wakulima pale bei za mazao yao zinaposhuka
chini ya gharama zao za uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu la uchaguzi
tumefanya mradi huu na hivi sasa wakulima wa kahawa wa vijiji vya Matyazo,
Mkabogo na Rusaba kupitia chama chao cha Ushirika cha RUMAKO ni wanachama wa
NSSF na tayari wameanza kufaidika na mafao kama bima ya afya na mikopo yenye
riba nafuu. Kufuatia mafanikio ya RUMAKO vyama vingine vya ushirika vinavyounda
chama kikuu cha KANYOVU chenye vyama 12 vya msingi wamejiunga na NSSF. Tunaweza
kusema kwa uhakika kabisa kuwa wakulima wote wa kahawa wa mkoa wa Kigoma
wanahifadhi ya Jamii kupitia vyama vyao vya ushirika. Shirika la NSSF sasa
limeanzisha mpango wa kuandikisha wakulima wengi zaidi nchi nzima kupitia
‘Wakulima scheme’. Katika mpango huu NSSF wameshirikiana na Tume ya Ushirika
nchini ambayo kuanzia january, 2014 imepewa jukumu la kudhibiti na kusimamia
vyama vya ushirika nchini. Ni hatua ya kupigiwa mfano. Hata hivyo bila vivutio
vya serikali wakulima hawatajiunga na hifadhi ya jamii kwa wingi tunaoutaka ili
kubadilisha kabisa uchumi wa watu wetu vijijini.
Mheshimiwa Spika, Napendekeza ifuatavyo
Serikali ianzishe mpango wa kuwachangia wakulima
wanaojiunga na Hifadhi ya Jamii kwa uwiano wa theluthi ya michango yao. Kwa
mfano iwapo mkulima atachangia tshs 20,000 kwa mwezi basi Serikali imchangie
tshs 10,000 kwa mwezi kwa sharti kwamba iwapo atajitoa kwenye hifadhi ya jamii
huu mchango wa Serikali hataupata lakini iwapo akikaa kwenye hifadhi ya jamii
kwa miaka isiyopungua kumi/umri wa kustaafu ataweza kupata michango yote na
mafao stahiki kwa mujibu wa sheria kama mfanyakazi wa sekta rasmi.
Serikali iachane na mpango wa kuanzisha ‘price
stabilisation fund’ na badala yake iweke sera kwamba wakulima waliokwenye
Hifadhi ya Jamii moja ya fao watakaolipata ni fao la fidia ya bei ambalo
litalipwa kwa namna ambayo wataalamu wa ‘actuarial’ wataona ni endelevu.
Serikali kupitia Msimamizi wa Hifadhi ya Jamii nchini
(SSRA) waelekeze kuwa mifuko itenge angalau 40% ya akiba wa wakulima kwenye
uwekezaji wa kuendeleza miundombinu ya kilimo, kuongeza thamani ya mazao ya
kilimo na kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima kupitia SACCOS/AMCOS
Mheshimiwa Spika, iwapo kwa mfano wakulima milioni moja
tu nchini walio kwenye vyama vya Ushirika wakijiunga katika hifadhi ya jamii na
kuchangia kiwango cha chini kabisa cha tshs 20,000 kwa mwezi (michango
itakayokatwa kulingana na msimu wa kilimo cha zao husika) na serikali kuweka
kivutio cha tshs 10,000 katika kila mchango wa mkulima mmoja mmoja katika idadi
hiyo, jumla ya Michango itakayokusanywa nitakuwa ni tshs 360 bilioni. Wakulima
hawa watapata bima ya afya wao, wenza wao na wategemezi 4 na hivyo bima ya afya
kufikia Watanzania milioni 6. Fedha hizi zitatumika kuwekeza kwenye miradi ya
uzalishaji katika sekta ya kilimo ikiwemo mikopo ya pembejeo, ujenzi wa
miundombinu ya kilimo na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaweza kuwekeza fedha hizi kama hisa kwenye Benki
ya Kilimo na kuwezesha uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo. Hii ndio
inaitwa ‘Transformation’.
Mheshimiwa Spika naomba kuwasilisha
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Kigoma Kaskazini.
Kigoma. Juni 17, 2014.
0 comments:
Post a Comment