RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ameyatupilia mbali madai
kwamba shambulizi la Mpeketoni lililoua watu zaidi ya 50 liliendeshwa na kundi
la Al shabab. Amesema kuwa shambulizi hilo ni la kikabila lililopangwa na
kuandaliwa vizuri kwa kuwahusisha wanasiasa wa ndani ya nchi hiyo.
“Kuna wanasiasa wa ndani ambao wamekuwa wakieneza
propaganda za kikabila na kampeni za chuki katika siku za hivi karibuni,”
alisema.
Katika hotuba yake kwa taifa hilo iliyorushwa moja kwa
moja na vituo vya televisheni, Rais Uhuru aliahidi kuwashughulikia wanasiasa
hao na wale wote waliozembea katika majukumu yao. “Maofisa wote wa usalama
waliozembea majukumu yao wakati wa shambulizi hilo wamesimamishwa na
watafikishwa mahakamani. Tabia hii haikubaliki kabisa,” alisisitiza Rais
Kenyatta.
"Ninawatolea wito Wakenya wote wasisahau tunu zetu
na wasisahau tulikotoka. Sitaruhusu kuona Kenya ikirudi tulikotoka,” aliongeza.
“Serikali yangu itafanya kazi kwa ajili ya Wakenya wote popote watakapokuwa,”
aliongeza katika kuhitimisha hotuba yake.
Alisema serikali yake itagharamia huduma zote za mazishi
ya wale walioathiriwa na shambulizi hilo.
0 comments:
Post a Comment