Maiti nane zimepatikana katika eneo la Poromoko karibu
na mji wa Mpeketoni nchini Kenya kufuatia mashambulizi mapya usiku wa kuamkia
leo. Nyumba kadhaa zimechomwa katika mashambulizi hayo, kwa mujibu wa polisi na
wakazi wa eneo hilo. Kuna taarifa kuwa kundi la Alshabaab, kupitia kituo chake
cha radio Andalus, kimedai kufanya shambulizi hilo na kwamba wamewaua watu 20. Idadi
ya vifo inaweza kuongezeka kwa kuwa polisi na wakazi wa eneo hilo wanaendelea
kutafuta miili mingine. Wakazi wengine wanasema kuwa nyumba zimechomwa katika
eneo la Mapenya usiku wa kuamkia leo.
Mkuu wa polisi nchini humo, David Kimaiyo, amethibitisha
ripoti za kugunduliwa maiti hizo lakini akasema kuwa haijulikani iwapo mauaji
hayo yametokana na mashambulizi mapya kama ilivyodaiwa na wakazi. Mpaka sasa
hakuna watu waliokamatwa kufuatia mauaji ya zaidi ya watu 50 yaliyofanywa na
watu wenye silaha usiku wa kuamkia jana katika eneo la Mpeketoni na Kibaoni.
Wakuu wa usalama wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani
Joseph Ole Lenku wako mjini Lamu na maafisa wengine wa usalama wamepelekwa
katika eneo hilo.
CHANZO: KTN
0 comments:
Post a Comment