Maandamano yamefanyika katika mji mkuu wa Ufaransa,
Paris, kutaka sheria ichukue mkondo wake dhidi ya askari wa Ufaransa
wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya ubakaji dhidi ya wakimbizi wakati wa mauaji
ya kimbari ya Rwanda miongo miwili iliyopita.
Waandamanaji hao wamechukua hatua hiyo huku jeshi la
Ufaransa likishtakiwa kwa ubakaji wa umati dhidi ya wakimbizi wa Rwanda, ambao
askari wa Ufaransa walitakiwa kuwalinda wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka
1994.
Mashitaka hayo yanaeleza kuwa askari katika kambi
iiyokuwa ikilindwa na wanajeshi wa Ufaransa walikuwa wakiwachagua wanawake wa Kitutsi
na kuwabaka zaidi ya mara moja.
Wanawake na askari hao hawajatangazwa hadharan, lakini
waathirika wameshatambuliwa mahakamani. Kesi hiyo imekuwa ikiendelea kwa zaidi
ya muongo mmoja sasa.
Mauaji ya kimbari ya Rwanda yalianza kufuatia
kutunguliwa kwa ndege ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Juvenal Habyarimana Aprili
6, 1994. Rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira naye aliuawa katika tukio hilo. Marais
wote wawili walikuwa kutoka kabila la Wahutu.
Baada ya tukio hilo, Wahutu ambao walikuwa wengi,
walianza kuwashambulia Watutsi. Mauaji hayo yalidumu kwa takriban siku 100
ambapo kiasi cha watu 800,000 waliuawa.
Mara kwa mara Ufaransa imekuwa ikikanusha kuhusika na
mauaji hayo ya kimbari licha ya uchunguzi wa tume ya MUCYO ya Rwanda uliofanyika
mwaka 2008 kubaini kuwa Ufaransa inadaiwa kutoa mafunzo kwa wapiganaji
waliotekeleza mauaji hayo.
0 comments:
Post a Comment