Jaji aliyemhukumu adhabu ya kifo kiongozi wa zamani wa
Iraq Saddam Hussein amekamatwa na kuuawa na wapiganaji wa kundi la Dola ya
Kiislamu katika Iraq na Sham (ISIS), imeelezwa.
Raouf Abdul Rahman, ambaye aliagiza Saddam anyongwe
mwaka 2006, ameripotiwa kuuawa na waasi kama kisasi kwa kifo cha Saddam
aliyenyongwa akiwa na umri wa miaka 69.
Kifo chake hakijathibitishwa na serikali ya Iraq, lakini
maofisa hawakukanusha taarifa zilizopatikana wiki iliyopita kwamba alikuwa
ametekwa. Inaaminika alikamatwa Juni 16 na kisha kuuawa siku mbili baadae.
Mbunge kutoka Jordan, Khalil Attieh, ameandika katika
ukurasa wake wa Facebook kuwa Jaji Rahman, aliyeongoza Mahakama Maalumu wakati
wa kesi ya Saddam, alitekwa na kuuawa.
“Wanamapinduzi wa Iraq walimkamata na kumuua katika
kulipiza kisasi kwa kifo cha marehemu Saddam Hussein,” aliandika, kama
alivyonukuliwa na mtandao wa Al-Mesyroon.
Aidha, Attieh alisema kuwa Jaji Rahman alijaribu
kutoroka kutoka bila mafanikio.
Vile vile ukurasa wa Facebook wa Izzat Ibrahim al-Douri,
ambaye alikuwa msaidizi wa Saddam na
ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa na ushawishi mkubwa miongozi mwa
waasi, aliandika kuwa waasi hao walikuwa wamemkamata Jaji Rahman.
Jaji Rahmann, ambaye alizaliwa katika mji wa Kikurd wa Halabja,
alichaguliwa kuongoza kesi hiyo mwezi Januari 2006 baada ya jaji wa mwanzo Rizgar
Amin kukosolewa kuwa alikuwa laini sana katika kumshughulikia Saddam na
washitakiwa wenzake.
Jaji huyo mwenye watoto watatu alihitimu masomo yake
katika shule ya sheria ya Chuo Kikuu cha Baghdad mwaka 1963 na kufanya kazi
kama mwanasheria kabla ya kuteuliwa kuwa jaji mkuu wa mahakama ya rufaa ya Kurdistan
mwaka 1996.
0 comments:
Post a Comment