Askari wa Israeli wamemteka
Spika wa Bunge la Palestina Aziz Dweik katika wimbi jipya la kamatakamata
inayoendelea kuhusiana na madai ya kutoweka kwa vijana watatu wa Kiyahudi.
Dweik, ambaye ni
mwanachama wa chama cha Hamas amekamatwa na jeshi la Israeli leo katika Ukingo
wa Magharibi.
Mpaka sasa zaidi ya
Wapalestina 150 wamekamatwa kwa kisingizo hicho cha kutoweka kwa vijana hao. Israel
inadai kuwa walitoweka siku ya Alhamisi katika eneo la Ukingo wa Magharibi na
kulituhumu kundi la Hamas kuwa limewateka.
Hamas imekanusha
madai ya Israel ikisema kuwa utawala wa Tel Aviv unakusudia kuhujumu mkataba wa
maridhiano uliofikiwa kati ya kundi hilo na chama cha Fatah uliopelekea kuundwa
kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa ikiyahusisha makundi yote ya Kipalestina.
Msemaji wa Klabu ya
Wafungwa wa Kipalestina, Amani Sarahna, amesema kuwa watu 60 walikamatwa jana,
akaongeza kuwa kamatakamata bado inaendelea katika katika mji wa al-Khalil
(Hebron) katika Ukingo wa Magharibi.
Mapema jana Jumapili,
vikosi vya Israeli viliwakamata viongozi wa Hamas Hassan Yousef, Wasfi Qabaha,
Khalid Abu Arafeh na Mohammed Totah.
Aidha, Israel imefunga
kivuko cha mpaka cha Kerem Shalom ambacho hutumika kupeleka nishati ya mfuta
katika eneo la Ukanda wa Gaza kufuatia kutoweka kwa walowezi hao. Kivuko cha Kerem
Shalom ndio njia pekee ambayo hutumiwa na magari ya mafuta kuingiza nishati
hiyo katika eneo hilo lililowekewa mzingiro.
0 comments:
Post a Comment