Rais wa Marekani Barack Obama kwa mara nyingine ameionya
Urusi kuhusu mgogoro wa Ukraine akisema kuwa Moscow inaweza kukabiliwa na maumivu zaidi kama hakutakuwepo na hatua madhubuti ya kuzuia hali ya mdororo na machafuko
inayoendelea katika taifa hilo lililokuwa sehemu ya Muungano wa Usovieti.
Ikulu ya Marekani imesema kuwa Obama alitoa onyo hilo
wakati akizungumza kwa njia ya simu na Rais wa Urusi Vladimir Putin jana
Jumatatu.
"Rais amezungumza na Rais Putin na kwa mara
nyingine amemtaka kuunga mkono amani badala ya kuruhusu usambazaji wa silaha na
zana kwenye mpaka na kusaidia waasi na wanaotaka kujitenga ambao wanaendelea
kuvuruga hali ya mambo nchini Ukraine,” msemaji wa Ikulu ya Marekani Josh
Earnest aliwaambia waandishi wa habari.
"Urusi itakabiliwa na gharama zaidi iwapo hatutoona
hatua madhubuti za kutuliza hali ya mambo,” alinukuu ujumbe wa Obama kwa Putin.
Wakati huohuo, Ikulu ya Urusi Kremlin imetoa taarifa
ikisema kuwa viongozi hao walijadili juu ya njia za kukomesha mzozo huo ambapo
Putin alisisitiza juu ya umuhimu wa kusimamisha mapigano nchini Ukaraine na
kuanzisha mazungumzo baina ya pande zinazozozana.
"Walijadili utekelezaji wa mpango wa amani
uliopendekezwa na Rais Petro Poroshenko (wa Ukraine)," ilisema taarifa ya Kremlin.
"Putin alisisitiza kwamba kipaumbele kinatakiwa kutolewa kwenye suala la
kusitisha operesheni za kijeshi na kuanza mazungumzo ya moja kwa moja baina ya
pande kinzani.”
Kiongozi huyo wa Urusi pia aliashiria juu ya masuala ya
kibinadamu, ikiwemo haja ya dharura ya kuwapelekea msaada raia walaioathiriwa
na mapigano mashariki mwa Ukraine.
Aidha, walijadili masuala ya kimataifa kama vila kadhia
ya Iraq, Syria, na programu ya nyuklia ya Iran.
Marekani na Urusi zimekuwa katika mzozo kuhusu eneo la
Crimea, ambapo Washington inaituhumu Moscow kuwa ilikuwa nyuma ya “kura haramu
ya maoni ya kujiondoa kwa Crimea” kutoka Ukraine na kuchochea machafuko
mashariki mwa nchi hiyo.
Moscow imeyakanusha madai hayo kwa kuyaita “yasiyokuwa
na maana” na kukana moja kwa moja kuhusika kwa vikosi maalumu vya Urusi kuchochea
ghasia nchini Ukraine.
0 comments:
Post a Comment