Kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 17, utawala wa Rais
Barack Obama umeidhinisha baadhi ya shughuli za kiserikali zisimamishwe kuanzia mapema leo baada ya Bunge la nchi
hiyo kuikataa bajeti yake, wakipinga mabadiliko ya kisheria ya sekta ya afya
yaliyofanyika hivi karibuni.
Huku matumaini ya suluhisho la mtafaruku huo wa bajeti
unaopambanisha wabunge wa chama tawala cha Democrat dhidi ya Republicans
yakizidi kufifia, wachumi na wataalamu wa uongozi wameonya kuwa uamuzi wa
kusitisha huduma ‘zisizo muhimu’ utaathiri uchumi wa Marekani kwa kiwango
kikubwa.
Wafanyakazi katika vitengo mbalimbali vya serikali
nchini humo waliodamkia maofisini leo alfajiri wamejikuta wakirudishwa
majumbani, huku karibu 800,000 kati yao wakiambiwa wachukue likizo bila malipo
mpaka muafaka utakapopatikana.
Wafanyakazi pekee watakaobakizwa ni wale ambao shughuli
zao haziwezi simama, kama vile madaktari na manesi, waongoza ndege na
wafanyakazi wa shirika la posta la Marekani.
Katika baadhi ya vitengo kama NASA – inayofanya tathmini
za usafiri wa kwenda sayari nyingine na anga za mbali – zaidi ya asilimia 95 ya
wafanyakazi wote wamewekwa benchi katika kipindi hiki cha mtafaruku wa bajeti.
Vilevile huduma za utoaji hati za kusafiri na viza
zinatarajiwa kusimama kwa kiwango kikubwa, na wasafiri toka nchi nyingine
wanaambiwa watarajie foleni ndefu kidogo katika vituo vya uhamiaji kwa sababu
wafanyakazi wengi wa kitengo hicho wamepumzishwa.
0 comments:
Post a Comment